Udhhiyah na swalah ya ´iyd kwa wanaoishi jangwani na mashambani

Sunnah na wajibu ni Udhhiyah iwe baada ya kuswali ya ´iyd akiwa mtu ndani ya mji. Lakini akiwa jangwani, kama vile mashambani, wachinje baada ya kuchomoza kwa jua. Jua likichomoza na kukapita muda kadhaa wa kiasi cha kuswaliwa, basi watachinja wakati huo. Watachinja baada ya kuchomoza kwa jua na kukapita kitambo kidogo cha kiasi cha kuswaliwa. Hapo ndipo watachinja, kwa sababu hawana swalah. Watu wa jangwani ni wasafiri na hivyo hawana swalah ya ´iyd. Kwa hivyo watachinja baada ya kuchomoza kwa jua.

Vivyo hivyo mahujaji wa Minaa ambao watachinja baada ya kuchomoza kwa jua, kwa sababu hawana swalah ya ´iyd Minaa. Kurusha vijiwe kunasimama mahali pa kuswali swalah ya ´iyd. Hivo ndivo alivofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alirusha vijiwe kisha akachinja kichinjwa chake cha Hadiy na hakuswali (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) swalah ya ´iyd katika hijjah ya kuaga. Kwa hivyo mahujaji watarusha vijiwe kisha wachinje chinjwa vyao baada ya wakati huo jua kuchomoza. Hayo ndio yamewekwa katika Shari´ah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/17196/حكم-الاضحية-في-عيد-الاضحى-وكيفيتها
  • Imechapishwa: 13/06/2024