Ubainifu wa ni lini mwanamke anasafika na hedhi yake

Swali: Mwanamke anapatwa na hedhi kwa muda wa siku kumi na tano. Kati ya hizo siku saba au nane hutokwa na damu nyeusi yenye harufu mbaya na siku zilizobaki hutoka damu ya manjano inayochanganyika na wekundu. Je, mwanamke huyu aache swalah siku kumi na tano zote au siku saba tu?

Jibu: Hedhi haina kiwango cha chini wala cha juu kwa mujibu wa maoni sahihi. Hakuna mpaka wa uchache wake wala wa wingi wake. Ikiwa ni ada yake siku kumi na tano, damu yake ikiwa baadhi ni nyeusi, baadhi ni ya manjano na baadhi ni nyekundu, basi katika siku zote hizo asiswali, hafungi na wala mume wake hamjamii mpaka atakaposafika.  Ama ikiwa anasafika kutoka kwenye damu, kisha baada ya twahara yakaja maji ya uchafuchafu na umanjano, hii haina hukumu ya hedhi. Maji ya uchafuchafu na umanjano baada ya twahara hazihesabiwi kuwa ni hedhi. Hivyo ataswali, atafunga na anahalalika kwa mume wake pamoja na maji ya uchafuchafu na umanjano. Lakini ikiwa maji ya uchafuchafu na umanjano kumeungana moja kwa moja na damu ya hedhi bila kupatikana twahara katikati, basi hiyo ni hedhi. Katika hali hii hatoswali wala kufunga. Lakini ikiwa alipata twahara kamili baada ya siku saba, nane au tano kwa mfano, kisha baada ya twahara hiyo yakaja maji ya uchafuchafu au umanjano, basi hiyo haina hukumu ya hedhi. Umm ´Atwiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Tulikuwa hatuzingatii umanjano na maji ya uchafuchafu kuwa ni kitu baada ya kusafika.”

Maana yake ni kwamba baada ya kuoga na kupata twahara iliyo wazi, kisha yakaja maji ya uchafuchafu au umanjano, katika hali hiyo hakuna jambo juu yake. Ataswali, atafunga na atahalalika kwa mume wake na atafanya kama anavyofanya mwanamke mwenye damu ya ugonjwa ikiwa ni pamoja na kutawadha baada ya kuingia wakati wa swalah na atajisitiri kwa pamba au mfano wake mpaka damu hiyo ikome.

Mwanafunzi: Je, inamlazimu kuoga?

Ibn Baaz: Hapana. Ni kama ilivyo kwa mkojo.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/2131/بيان-متى-تطهر-المراة-من-حيضها
  • Imechapishwa: 24/07/2026