Tunatoaje zakaah ya vito vya wake zetu?

Swali: Tunatoaje zakaah ya dhahabu ya wanawake?

Jibu: Inatolewa kama inavyotolewa zakaah ya mali nyingine, robo ya kumi. Kuhusu dhahabu, inatolewa robo ya kumi hata ikiwa inavaliwa. Maoni sahihi ni kuwa inatolewa zakaah hata kama inavaliwa. Ikifika kiwango kinachotakiwa kutolewa zakaah, basi hutolewa robo ya kumi ya thamani ya mapambo ya dhahabu, pete, mkufu, bangili na mengineyo. Inajulikana uzito wake sokoni, kisha inatolewa kwa thamani yake ya sokoni ya dhahabu inayojulikana. Hii ikiwa ni dhahabu na fedha. Ama vito vingine kama almasi na aina nyingine za mapambo yasiyo dhahabu au fedha, hayo hayana zakaah ikiwa ni kwa ajili ya kuvaa, si kwa ajili ya kuuza wala biashara. Havina zakaah.

Mwanafunzi: Hata kama haijaandaliwa kwa biashara?

Ibn Baaz: Hata kama haijaandaliwa kwa biashara. Haya ndio maoni sahihi zaidi katika maono ya wanazuoni. Ikiwa imefikia kiwango kinachowajibika kutoa zakaah, nayo ni Mithqaal ishirini za dhahabu, sawa na jedi kumi na moja na theluthi tatu za jedi moja. Hicho ndiyo kiasi chake.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/993/كيفية-زكاة-حلي-النساء
  • Imechapishwa: 05/01/2026