Tofauti yetu na al-Ikhwaan al-Muslimuun sio kama tofauti zilizokuwepo kati ya Ahmad na ash-Shaafi´iy, au ash-Shaafi´iy na Maalik. Tofauti yetu sio kutamka jina la Allaah kwa sauti ya juu kabla ya al-Faatihah au kutamka kimyakimya, au kama inafaa kula kichinjwa kilichotajiwa jina la Allaah au haifai kukila, kuanza kutaja jina la Allaah kabla ya kutawadha au kutotaja. Makinzano yetu ni katika mambo ya ´Aqiydah. Ingawa makinzano ya pili sio mepesi, angalau ni tofauti zinazohusiana na utekelezaji wa ´ibaadah mbalimbali, kama vile kusoma Tashahhud kwa njia mbalimbali, kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia mbalimbali na uelewa mwingine mbalimbali. Hayo yalikuwepo hata wakati wa Maswahabah. Lakini makinzano yaliyokemewa naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah ni yale ya kugongana. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtembelea bwana mmoja mgonjwa akasema:

لا بَأْسَ، طَهُورٌ إنْ شاءَ اللَّه

“Hapana neno. Ni utakaso – Allaah akitaka.”

Bwana yule akasema: “Hapana hata kidogo. Ni homa kali kwa mzee ambaye yuko njiani kuelekea makaburini.” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: “Basi iwe hivyo.”[1]

Salamah bin Akwa´ amesema:

“Mtu mmoja alikula kwa mkono wake wa kushoto mbele ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema: “Kula kwa mkono wako wa kulia.” Akasema: “Siwezi.” Ndipo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Basi kamwe hutoweza.” Hakuna kilichomzuia isipokuwa ni kiburi. Kisha baada ya hapo hakuweza tena kuupandisha kinywani mwake.”[2]

Tofauti ya kugongana ilikaripiwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake.

[1] al-Bukhaariy (5662).

[2] Muslim (2021).

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Mu´aanid, uk. 105-106
  • Imechapishwa: 12/02/2025