80. Tofauti ya uombezi mbele ya Allaah na mbele ya viumbe

Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

وإن رَسُولَ اللهِ للخَلْقِ شَافِعٌ

32 – Hakika Mtume wa Allaah ni muombezi wa walimwengu

وقُلْ في عَذابِ القَبْرِ حَقّ موُضحُ

     Sema kuhusu adhabu ya kaburi kwamba ni haki na iliyowekwa wazi

MAELEZO

Mtunzi (Rahimahu Allaah) katika shairi hili ametaja mambo mengi:

1 – Maswali ya Malaika wawili.

2 – Adhabu na starehe za ndani ya kaburi.

3 – Kupimwa kwa matendo.

4 – Hodhi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

5 – Suala kuhusu waislamu wenye kutenda dhambi kubwa.

6 – Suala la kuhusu uombezi. Uombezi pia umetajwa katika shairi hili.

Uombezi maana yake ni ule ukatikati unaokuwepo katika kutatua haja mbalimbali kutoka kwa yule mwenye nao. Uombezi unakuwa kwa Allaah na kadhalika kwa watu. Uombezi uliyopo kwa Allaah unatofautiana na uombezi uliyopo kati ya watu. Unaweza kuombea mbele ya mtu hata kama mtu huyo hakukupa idhini. Kuhusu Allaah (Jalla wa ´Alaa) hakuna yeyote awezae kuombea mbele Yake isipokuwa baada ya kupata idhini Yake:

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?” (02:255)

Yeye ndiye humpa idhini muombeaji aombee. Ni lazima yule muombewaji awe ni katika watu wa Tawhiyd au kwa msemo mwingine awe ni katika wale waislamu watenda madhambi waliokuwa wakimuabudu Allaah peke Yake. Ama kuhusu kafiri hana uombezi wowote juu yake na uombezi haukubaliwi kwake:

مَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ حَمِيمٍ وَلَا شَفِيعٍ يُطَاعُ

“Madhalimu hawatokuwa na rafiki wa dhati na wala mwombezi anayetiiwa.” (40:18)

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ

“Basi hautowafaa uombezi wowote wa waombezi.” (74:48)

Kafiri uombezi juu yake haukubaliwi:

وَاتَّقُوا يَوْمًا لَّا تَجْزِي نَفْسٌ عَن نَّفْسٍ شَيْئًا وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا عَدْلٌ وَلَا تَنفَعُهَا شَفَاعَةٌ و

“Na iogopeni siku ambayo nafsi haitoifaa nafsi nyingine chochote wala haitokubaliwa kutoka kwake kikomboleo wala hautamfaa uombezi” (02:123)

Lau kafiri atatoa mali zote za duniani anataka fidia hazitokubaliwa kwake:

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَمَاتُوا وَهُمْ كُفَّارٌ فَلَن يُقْبَلَ مِنْ أَحَدِهِم مِّلْءُ الْأَرْضِ ذَهَبًا وَلَوِ افْتَدَىٰ بِهِ

“Hakika wale waliokufuru na wakafa nao wakiwa makafiri, basi haitakubaliwa kutoka kwa mmoja wao [fidia ya] dhahabu ya kujaza dunia nzima lau wakitaka kujikombolea nayo.” (03:91)

Fidia ili wazikomboe nafsi zao haitokubaliwa kutoka kwao. Hakuna uombezi wa yeyote utakubaliwa juu yao. Wao bila ya shaka yoyote kabisa ni katika watu wa Motoni ambapo watadumishwa humo milele. Uombezi mbele ya Allaah hauthibiti isipokuwa kwa kutimia sharti mbili:

1 – Allaah ampe idhini mwombezi aombee.

2 – Muombewaji awe ni katika waislamu watenda maasi waliokuwa wakimuabudu Allaah peke Yake.

Kuhusiana na viumbe unaweza kuombea mbele yao hata kama hawakukupa idhini ya kufanya hivo na hata kama mtu huyo hayuko radhi kwa yule unayemuombea. Bali kuna uwezekano mtu huyo akawa na chuki kwa yule unayemuombea na anatamani hata kumuua au kumpatiliza. Lakini hata hivyo akawa hana budi kukubali uombezi juu yake kwa kutenzwa nguvu kutokana na ile haja alio nayo kwa watu, mawaziri na wasaidizi. Endapo hatokubali uombezi wao watamkaripia. Kwa hivyo anakuwa hana budi kuwafanyia upole na kukubali uombezi wao japokuwa hakutoa idhini na hayuko radhi kwa yule muombewaji. Ama Allaah (Jalla wa ´Alaa) hakuna yeyote awezae kuombea mbele Yake isipokuwa kwa idhini Yake na hakuna yeyote anayeombewa Kwake isipokuwa tu wale waislamu watenda dhambi wenye kumuabudu Yeye peke yake. Hii ndio tofauti kati ya nyombezi hizo aina mbili.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 172-173
  • Imechapishwa: 13/01/2024