Tofauti ya kutumainia kheri na kuamini mkosi

Swali: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kuboresha majina. Je, hilo linaingia katika kuamini mkosi?

Jibu: Hapana, hili si katika kuamini mkosi. Bali ni katika mlango wa kutumainia kheri (الفأل). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipenda al-Fa´l. Ama kuamini mkosi ni mtu kuacha jambo lake kwa sababu ameona kitu anachokichukia au amesikia kitu anachokichukia; akaliacha jambo lake kwa sababu hiyo au akafanya jambo ambalo hakulitaka kwa sababu hiyo. Ndiyo maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote ambaye mkosi wa ndege umemrudisha katika haja yake, basi amefanya shirki.”

Nayo ni shirki ndogo.

Mkosi ni katika shirki ndogo. Inaweza kuwa shirki kubwa ikiwa ataamini kuwa kitu anachokitolea nuksi kina uwezo wa kuathiri, kina uendeshaji katika ulimwengu bila ya Allaah, kinaweza kunufaisha au kudhuru au akakielekezea aina fulani ya ´ibaadah. Kama vile akielekeza ´ibaadah kwa nyota fulani anayoiamini, kama Miriykh au Thurayyaa au kwa mnyama fulani, kwa sanamu fulani au kwa maiti fulani, basi hilo linakuwa shirki kubwa. Ama kujisikia ubaya moyoni na kuchukia jambo kisha akaacha au akaendelea nalo kwa sababu hiyo, hili ni jambo la kiasili linalopatikana katika nafsi. Halina athari ya kweli. Hili ni katika shirki ndogo isipokuwa ikiwa ataamini yale yanayolifanya kuwa shirki kubwa, kama kuamini kuwa kina uwezo wa kuyaendesha katika mambo ya watu na maisha yao au akakielekezea baadhi ya ´ibaadah. Katika hali hiyo inakuwa ni shirki kubwa.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3219/الفرق-بين-الفال-والتطير
  • Imechapishwa: 20/10/2026