Tofauti ya Ahl-us-Sunnah na Ahl-ul-Bid´ah juu ya viongozi madhalimu

Imaam at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hatuonelei kufanya uasi kwa viongozi na watawala wetu hata kama watafanya unyanyasaji. Vilevile hatuombi du´aa dhidi yao na hatujivui kutoka katika utiifu wao. Badala yake tunaonelea kuwatii ni katika kumtii Allaah (´Azza wa Jall) na ni faradhi midhali hawajaamrisha maasi. Tunawaombea kunyooka.”

Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hawaonelei kufanya uasi kwa watawala kwa sababu ya maasi hata kama watafanya unyanyasaji na kudhulumu. Vilevile hatujivui kutoka katika utiifu wala [hatuonelei] kuwachochea watu kuwafanyia uasi. Tunawaombea kunyooka na hatuwaombei du´aa dhidi yao. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah tofauti na Ahl-ul-Bid´ah miongoni mwa Khawaarij na Mu´tazilah na Raafidhwah. Hii ndio sababu ya mwandishi (Rahimahu Allaah) na wengine kuingiza haya katika vitabu vya ´Aqiydah.

Khawaarij wanaona kusihi kufanya uasi kwa mtawala kwa sababu ya maasi. Mtawala akifanya maasi wanaona kuwa ni kafiri na inafaa kumuua na kumg´oa katika uongozi. Haya ni madhehebu batili.

Vilevile Mu´tazilah wanaona kuwa mtawala akitenda dhambi kubwa kama kunywa pombe basi ni wajibu kumfanyia uasi kwa sababu ametoka katika imani na kuingia katika kufuru na kumdumisha Motoni.

Kadhalika Raafidhwah wanaona kusihi kumfanyia uasi mtawala kwa sababu ya maasi kwa kuwa wanaona kuwa uongozi wake ni batili. Bali wao hawaonelei kuwepo kwa uongozi isipokuwa yule kiongozi ambaye amekingwa na kukosea. Ama viongozi wengine uongozi wao ni batili. Maimamu waliokingwa na kukosea ni wale kumi na mbili ambao ameteuliwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – kama wanavyodai. Wamewapanga ifuatavyo:

1- ´Aliy bin Abiy Twaalib.

2- al-Hasan bin ´Aliy.

3- al-Husayn bin ´Aliy.

Kisha maimau waliosalia tisa wote ni katika kizazi cha al-Husayn bin ´Aliy:

4- Zayn-ul-´Aabidiyn.

5- Muhammad bin ´Aliy al-Baaqir.

6- Ja´far bin Muhammad as-Swaadiq.

7- Muusa bin Ja´far al-Kaadhwim.

8- ´Aliy bin Muusa ar-Ridhwaa.

9- Muhammad bin ´Aliy a-Jawaad.

10- ´Aliy bin Muhammad al-Haadiy.

11- al-Hasan bin ´Aliy al-´Askariy.

12- Imamu wa kumi na mbili ni Muhammad bin al-Hasan al-Khalf al-Hujjah al-Mahdiy anayesubiriwa ambaye ameingia pangoni Samraaa´ huko ´Iraaq 260 na hajatoka mpaka hii leo.

Hawa ndio maimamu walioteuliwa kwao. Mbali na hawa uongozi wao ni batili na ni wajibu kuwatoa katika uongozi wao kukiwepo uwezo wa kufanya hivo.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (02/546-548)
  • Imechapishwa: 19/05/2020