Swali: Mtunzi wa kitabu ametaja kwamba hekima ya kuchelewesha swalah ya Dhuhr hadi kupungue joto ni kwa ajili ya kupunguza ukali wa joto, lakini siku hizi kuna viyoyozi vingi?

Jibu: Hiyo ndiyo asili, kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ikiwa joto litakuwa kali, basi chelewesheni swalah, kwani ukali wa joto unatokana na upumuaji wa Jahannam.”

Swali: Sasa hivi kuna viyoyozi vingi?

Jibu: Haijalishi kitu, kwa sababu barabarani bado kuna joto. Mtu anapotoka kuelekea msikitini anapata joto, joto baada ya baridi na baridi baada ya joto – mwili unaathirika.

Swali: Lakini inapokuja katika suala la adhaana mfano wakichelewesha inaweza kuwachanganya misikiti mingine?

Jibu: Kwa hali yoyote wakikubaliana kuchelewesha adhaana ndio bora zaidi, kwani Sunnah ni kuchelewesha adhaana. Lakini kama hawataichelewesha, basi wanaweza kuchelewesha Iqaamah. Hata hivyo ni bora zaidi kuchelewesha adhaana pia, kwa sababu watu wanaposikia adhaana, huanza kujiandaa. Kwa hivyo ni bora adhaana icheleweshwe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa safarini alipoambiwa na muadhini kuwa ataadhini, alisema:

“Chelewesha, chelewesha, chelewesha.”

Mpaka walipoona kivuli kimeanza kutoka nyuma ya vilima, ndipo akamuamuru aadhini.

Swali: Ikiwa nyakati za adhaana zimepangwa rasmi – je, bado wanaruhusiwa kuchelewesha?

Jibu: Hapana, wakishapangiwa nyakati, wanapaswa kuzifuata. Kwa sababu kuchelewesha kutaweza kusababisha migongano na mizozo. Hivyo makubaliano baina yao ni bora kuliko mzozo.

Swali: Hadiyth inayosema kwamba Jahannam huchochewa moto wake wakati huo?

Jibu: Ni Swahiyh. Hiyo ni sababu nyingine, kwani Jahannam huchochewa moto wake wakati wa joto kali. Ndani yake kuna hekima ya kuwafanyia wepesi waislamu na kuwasaidia kuswali kwa unyenyekevu wa moyo. Kwa hiyo ukali wa joto unatokana na kuchochewa kwa Jahannam na tiba ya joto kali ni kuchelewesha swalah ya Dhuhr.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/31140/هل-تنتفي-علة-الابراد-بالصلاة-مع-وجود-المكيفات
  • Imechapishwa: 06/10/2025