Swali: Khatwiyb alichelewa kufika siku ya ijumaa. Mmoja wa waswaliji akapanda mimbari na akasoma Suurah Qaaf katika Khutbah ya kwanza, kisha katika Khutbah ya pili akaomba du´aa fupi, halafu akashuka chini. Ni ipi hukumu ya Khutbah hii?

Jibu: Hakuna ubaya katika hilo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitoa Khutbah kwa kusoma Suurah Qaaf. Mmoja wa Maswahabah wa kike (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Sikuihifadhi Suurah Qaaf isipokuwa kutoka kwenye ulimi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); alikuwa akiisoma kila ijumaa akiwa juu ya mimbari.”

Kwa hiyo ikiwa Khatwiyb atamhimidi Allaah, atamtukuza, atamswalia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), atawausia waislamu wamche Allaah, kisha akasoma Suurah Qaaf, basi hayo yatakuwa ni mawaidha makubwa.

Vilevile Khutbah ya pili huianza kwa kumhimidi Allaah, kutoa ushahidi wa kumpwekesha Allaah (Ta´ala), na kutoa ushahidi kwamba Mtume Wake ni Mjumbe Wake, kisha humswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), huwaamrisha watu wamche Allaah, kisha hukamilisha Khutbah yake.

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Mutanawwi´ah (24)
  • Imechapishwa: 16/09/2026