Swali: Tunasikia baadhi ya washabiki wa makundi wanasema kusizungumziwe matatizo ya Ummah; kama Shirki, Zinaa na mambo mengine katika Bid´ah na maasi. Mambo haya yanaufarikanisha Ummah.

Jibu: Kwani sisi tunataka Ummah uwe na umoja juu ya upotevu? Sisi tunataka Ummah uwe na umoja juu ya haki. Ummah hauwezi kuwa na umoja isipokuwa juu ya haki. Ama kuwa na umoja juu ya batili, Ummah kamwe hauwezi kuwa na umoja. Haki ndio inayowafanya watu kuwa na umoja. Ama batili inawafarikanisha watu.

Huku ni kuufanyia ghushi Ummah. Kunyamazia maovu, mapungufu ambayo yanaiharibu ´Aqiydah, Dini na murua, hii ni ghushi tofauti na nasaha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Dini ni kupeana nasaha.” Tukasema: ”Ni kwa nani, ewe Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Kwa Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake, viongozi wa Waislamu na watu wa kawaida.”

Muislamu ni yule mwenye kuwanasihi ndugu zake kwa kuwabainishia yale yenye kuwadhuru na kuwapendezeshea yale yenye kuwanufaisha. Huyu ndio mnasihiaji. Ama yule mwenye kunyamaza juu ya makosa ya watu yanayohusiana na ´Aqiydah na matamanio yao, anawanyamazia na wala hayasahihishi, huyu ni mwenye kufanyia ghushi Ummah. Isitoshe mtu kama huyu anaufarikanisha Ummah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab Ahaadiyth-il-Fitnah (2) http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/ftn–1432-08-16.mp3
  • Imechapishwa: 21/04/2015