Si kila anayeishi Ulaya ni muharibifu na hafai kuozwa

Swali: Vijana wengi – isipokuwa aliowalinda Allaah – husafiri sana kwenda nje ya nchi. Mnafahamu yanayowapata huko kama uzinifu na unywaji wa pombe. Iwapo mmoja wa vijana hawa atakuja kuchumbia na ikaonekana juu yake dalili za wema, je, anaozeshwa ilihali Allaah amesema:

الزَّانِي لَا يَنكِحُ إِلَّا زَانِيَةً أَوْ مُشْرِكَةً

“Mwanamme mzinifu hafungi ndoa isipokuwa na mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina.”[1]

Jibu: Si kila kijana anayesafiri kwenda nje ya nchi huwa ni muharibifu. Huenda baadhi ya vijana wakawa miongoni mwa watu wema zaidi, hata kama wako nje ya nchi. Huenda wakaanzisha jumuiya, wakafanya matendo mema na wakawa ni walinganizi wa dini ya Allaah kwa namna inayofurahisha nyoyo. Huenda hata hali yao ikawa bora zaidi kuliko walivyokuwa katika nchi zao. Lakini wengi wao hubadilika na kuharibika. Wengi wanaosafiri kwenda nje, kama Uingereza, Ufaransa au Marekani, hali yao hubadilika na kuelekea kwenye uharibifu. Hali hii ndiyo iliyoenea zaidi miongoni mwao katika dini na maadili yao – tunamuomba Allaah atujaalie usalama. Kwa hiyo ikiwa hakuonekana juu yake uharibifu, basi anaozeshwa. Ikiwa alikuwa na uharibifu kisha akatubia na zikadhihiri juu yake dalili za tawbah, basi aozeshwe. Tawbah hufuta yaliyoitangulia.

[1] 24:03

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/2115/حكم-نكاح-من-يخاف-وقوعه-في-الزنا
  • Imechapishwa: 27/03/2026