Safari ya Mtume kwenda mbinguni inathibitisha ujuu wa Allaah

49- Ibn ´Abbaas amesema:

”Je, mnashangazwa urafiki wa ndani uwe kwa Ibraahiym, maneno iwe kwa Muusa na kuonekana iwe kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?”[1]

Hadiyth hii vilevile inathibitisha kuwa Allaah (Subhaanah) yuko juu ya mbingu na juu ya viumbe wote. Kama isingelikuwa hivyo, basi ingelikuwa haina maana yoyote Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kusafirishwa sehemu ya usiku mpaka mbingu ya saba kwenye mkunazi wa mwisho na Allaah akamsogele – usogeleaji Wake (Subhaanah) hautakiwi kufanyiwa namna – mpaka akawa ni kama baina ya mipinde miwili au karibu zaidi kutoka Kwake, na kwamba alimuona usiku huo na kwamba Jibriyl alipanda naye mpaka akafika naye kwa Allaah (Ta´ala) na kwamba mambo yote haya yanafidisha ya kwamba yuko juu ya mbingu. Yote haya hayana maana yoyote kwa mujibu wa wale wanaosema kuwa Allaah yuko kila mahali kwa dhati Yake kukiwemo vyooni, matumbo, vifuko vya kizazi na vingine vyote vinavyotofautiana na maumbile ya mwanaadamu ambayo Allaah amemuumba kwayo. Allaah amewaumba wanaadamu na maumbile ya kutambua kuwa yuko juu ya ´Arshi na juu ya mbingu saba. Amewatuma Mitume kuthibitisha hilo. Hakuwatuma kuthibitisha kuwa hayuko juu ya ´Arshi wala ya kwamba yuko ndani ya ulimwengu au nje ya viumbe.

[1] Ibn Abiy ´Aaswim (1/192). al-Albaaniy amesema: ”Mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh na ni kwa mujibu wa masharti ya Muslim.”

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-´Arsh (2/53-55)
  • Imechapishwa: 11/04/2017