Sababu zinazofanya mtu kuwa na unyenyekevu ndani ya swalah

Swali: Ni ipi sababu ipi inayofanya mtu kutokuwa na unyenyekevu ndani ya swalah? Ni vipi mtu atajinasua na hali hiyo?

Jibu: Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ

“Hakika wamefaulu waumini; ambao katika swalah zao ni wenye kunyenyekea.”[1]

Kuna sababu mblimbali zinazofanya kuwa na unyenyekevu kama ambavo pia kuna sababu zinazofanya mtu asiwe na unyenyekevu. Unyenyekevu una sababu ikiwa ni pamoja na kunyenyekea mbele ya Mola na ukumbuke kuwa umesimama mbele Yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Imepokelewa katika Hadiyth Swahiyh:

“Atapopiga Takbiyr mmoja wenu basi asiguse kokoto. Kwani rehema inamkabili.”[2]

Katika tamko jengine imekuja:

“Ataposimama mmoja wenu ndani ya swalah basi hakika anamnong´oneza Mola Wake.”[3]

Mtu anapoingia ndani ya swalah basi hakika anamnong´oneza Mola Wake. Hivyo akumbuke nafasi hii tukufu na kwamba yuko mbele ya Allaah. Kwa hivyo anyenyekee kwa Allaah, aelekee swalah yake, akumbuke utukufu wa Allaah, kwamba yuko mbele ya Mtukufu wa watukufu (Jalla wa ´Alaa), aielekee swalah yake, kisomo chake, Sujuu na Rukuu´ yake, akumbuke kila kinachopelekea nafasi hii na kwamba kupumbaa kwake juu ya Allaah kunaitia dosari swalah yake. Anatakiwa ayakumbuke hayo ili kumwondokee ule upumbaaji na wasiwasi. Aidha amwombe Allaah msaada juu ya hayo katika Sujuud yake na mwishoni mwa at-Tahiyyaat aombe kwa kusema:

اللهم أعني على الخشوع، اللهم يسر لي الخشوع، اللهم أَعِذْني من الشيطان ومن شرِّ نفسي

“Ee Allaah! Nisaidie juu ya unyenyekevu! Ee Allaah! Niwepesishie mimi unyenyekevu! Ee Allaah! Nilinde mimi na shaytwaan na shari na nafsi yangu!”

Amwombe na kumtaka msaada Mola Wake.

[1] 23:01-02

[2] at-Tirmidhiy (346) na an-Nasaa´iy (1178).

[3] al-Bukhaariy (390), Muslim (856) na Ahmad (4673).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/264)
  • Imechapishwa: 02/11/2021