Ruhusa ya wazazi kwa ajili ya kwenda kuhiji

Swali 63: Je, ni lazima kuomba ruhusa kwa wazazi katika kwenda kuhiji, ni mamoja iwe ni Hijjah ya faradhi au ya Hijjah kujitolea?

Jibu: Ama ikiwa ni faradhi, basi hakuhitajiki ridhaa yao wala ruhusa yao. Bali kama wakimzuia kuhiji huku Hijjah hiyo ni faradhi, basi ni wajibu kwake kuhiji wala asiwatii. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا

“Wakikufanyia juhudi kwamba unishirikishe na yale usiyokuwa na elimu nayo, basi usiwatii. Lakini suhubiana nao kwa wema duniani.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba.”[2]

Lakini ikiwa ni Hijjah ya kujitolea, basi aangalie maslahi. Ikiwa baba yake na mama yake hawawezi kuvumilia kuwa mbali naye wala hawawezi kustahamili kutokuwepo kwake, basi kubaki kwake pamoja nao ni bora zaidi. Kwa sababu mtu mmoja alimwomba ruhusa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenda jihaad ambapo akamuuliza:

“Je, wazazi wako wawili wako hai?” Akasema: Ndiyo. Akasema: “Basi kwao wawili fanya jihaad.”[3]

Kwa hiyo katika faradhi hawatakiwi kutiiwa. Lakini katika jambo la kujitolea huangaliwa lile lenye manufaa zaidi.

[1] 31:15

[2] Ahmad (1/131) na al-Haakim (2/314). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (7520).

[3] al-Bukhaariy (3004) na Muslim (2549).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (21/67)
  • Imechapishwa: 02/06/2026