Enyi watu! Jiandaeni na safari; hakika mmepatwa na wasiwasi. Yatibuni maradhi yenu; kwani hakika mna uwezo wa kufanya hivo. Hakika mwezi huu ndio mwezi bora kabisa. Ni wenye kufungua vifua vilivyofungwa,  unaokoa kutoka mitego ya madhambi na una usiku ambao kunakadiriwa kila jambo. Allaah ameufadhilisha zaidi ya miezi elfu na kusema:

سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ

”Ni amani mpaka kuchomoza alfajiri!”[1]

Hakuna yeyote mwenye kuomba du´aa katika usiku huo isipokuwa hujibiwa, hakuna yeyote anayetubia katika usiku huo isipokuwa husamehewa na kukubaliwa. Liko wapi jicho linalotazama kwa mazingatio? Wako wapi wenye kutafakari kwa tafakuri za kweli? Ziko wapi fikira za kufikiria namna unavyoenda usiku na mchana? Hivi mmesahau maneno ya Mjuzi wa kuyajua ya yenye kuonekana na yaliyojificha:

يَا قَوْمِ إِنَّمَا هَـٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا مَتَاعٌ وَإِنَّ الْآخِرَةَ هِيَ دَارُ الْقَرَارِ

“Enyi watu wangu! Hakika maisha haya ya dunia ni starehe ya kupita tu na hakika Aakhirah ndiyo nyumba ya kutulizana milele.”[2]

Ee wewe ambaye umeghurika kwa mipango ya muda mrefu! Ee wewe ambaye umeghafilika kwa muda wa kufa kwako! Hakika huu ni wakati wa kujipinda kikwelikweli na mtu kujiandaa kwa ajili ya siku ya Qiyaamah. Sasa zinapita siku ambazo pengine hutorudi tena kuzipata kwa mara nyingine. Sasa kunapita mwezi ambao pengine hutorudi tena kuupata. Allaah amrehemu mtu ambaye amezinduka kutoka kwenye usingizi wa matamanio yake na akaichagulia nafsi yake maisha mazuri kabla ya majuto na kabla ya kukubaliwa udhuru wowote; kabla ya mipango ya mustakabali yenu hayajapotea, kabla ya ujenzi wa maisha yenu hayajadhoofika, kabla ya miili yenu mipya haijaoza na kabla ya tetesi zenu kusahaulika na kupotea! Naapa kwa Allaah, enyi wajinga, kwamba hii ndio njia mnakoelekea! Karibuni mtazikwa. Karibuni mtafufuliwa kutoka nje ya makaburi yenu kwenda kukutana na Mola wenu, kusimama mbele Yake na kuulizwa:

أَفَسِحْرٌ هَـٰذَا أَمْ أَنتُمْ لَا تُبْصِرُونَ

”Je, ni huu ni uchawi? Au nyinyi hamuoni?”[3]

فَوَرَبِّ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ إِنَّهُ لَحَقٌّ مِّثْلَ مَا أَنَّكُمْ تَنطِقُونَ

”Basi Naapa kwa Mola wa mbingu na ardhi! – hakika hiyo ni haki kama jinsi mnavyotamka.”[4]

[1] 97:5

[2] 40:39

[3] 52:15

[4] 51:23

  • Mhusika: Imaam Swiddiyq Hasan Khaan al-Qanuujiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Maw´idhwah al-Hasanah, uk. 107-108
  • Imechapishwa: 15/05/2020