Oa mke mwengine na umwache mama wa watoto wako kwa wazazi wako

Swali: Nafanya kazi Riyaadh  na mke wangu pamoja na watoto wanaishi kwa wazazi wangu Jiyzaan. Nataka niwalete kwangu, lakini wazazi wanakataa. Nami naogopa kuwakasirisha. Nifanye nini?

Jibu: Ni juu yako kujitahidi kupata ridhaa yao. Huenda wakakubali mke wako ahamie kwako, kwa sababu unamhitaji mke wako. Jitahidi na tumia watu wema waingilie kati ili kuwashawishi. Ikiwa mama yako ana uwezo wa kumhudumia baba yako na kumtimizia mahitaji yake, basi hilo ni jambo jingine. Ama ikiwa hawezi na baba yako anamhitaji mke wako na pia mama yako, basi mwache mke wako akae nao, nawe uvumilie.

Ikiwa una uwezo wa kuoa mke mwingine, basi oa. Oa mke mwingine umweke Riyaadh nyumbani kwako na umuache mama wa watoto wako kwa wazazi wako ikiwa wanamhitaji au hawaridhii aondoke. Hivyo utakuwa umeunganisha maslahi mawili: kuwafurahisha wazazi wako na mke wako kuwahudumia, kisha uoe mwingine ikiwa unaweza, hata kwa deni na Allaah atakulipia. Uoe mwanamke mwema huko Riyaadh atakayekuhudumia. Utakapokwenda kule kwa wazazi utarudi kwa mke wako wa kwanza, hakuna ubaya katika hilo. Usiwakasirishe wazazi wako na wala usiwadhuru, khaswa ikiwa wanamhitaji mke wako kwa sababu ya uzee wao. Ama ikiwa hawamhitaji, basi tafuta watu wa kuwapatanisha kati yako na wao ikiwa huwezi kuoa. Ikiwa unaweza kuoa, basi himdi zote ni za Allaah. Oa, kwani unaruhusiwa kuoa hadi wake wanne na mama wa watoto abaki kwa wazazi wako.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3228/حكم-طاعة-الوالدين-في-ابقاء-الزوجة-والاولاد-عندهم
  • Imechapishwa: 18/10/2026