Swali: Kikosi cha watu kinakusanyika juu ya madhambi makubwa, ikiwa ni pamoja na kuua, kupora, kuiba, kunywa pombe na mengineyo. Shaykh mmoja ambaye anatambulika kwa kheri na kufuata Sunnah akakusudia kuwakataza watu hao kutokamana na mambo hayo na hakuweza kuwafikia kwa njia nyingine isipokuwa kwa nyimbo na kwa nia hii. Kulipigwa matari na kukaimbwa mashairi yanayoruhusiwa pasi na vipengele vyovyote vya ujana. Baada ya yeye kufanya hivo vijana wengi walitubia. Matokeo yake akawa yule ambaye haswali wala hatoi zakaah na pia anaiba sasa anajiepusha na mambo yenye utata, anatekeleza mambo ya faradhi na anajiepusha na mmbo ya haramu. Je, inaruhusiwa kwa Shaykh huyu kuimba kwa njia hii kutokana na yale manufaa yanayopelekea katika jambo hilo na kwamba hawezi kuwalingania kwa njia nyingine isipokuwa hii tu?

Jibu: Shaykh aliyetajwa kushindwa kuwafanya watenda madhambi makubwa wakatubia isipokuwa kwa njia ya mfumo uliyozuliwa ambao umetajwa katika swali, ni dalili inayofahamisha kuwa Shaykh huyo ni mjinga wa mifumo iliyowekwa katika Shari´ah ambayo kwayo wanasamehewa watenda madhambi makubwa au mifumo hiyo imemshinda. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah na wanafunzi wa Maswahabah walikuwa wakiwalingania walio waovu zaidi kuliko watu hawa – katika makafiri, watenda madhambi na maasi – na walifanya hivo kwa kutumia zile njia zilizowekwa katika Shari´ah. Allaah aliwatosheleza nazo kutokamana na mifumo iliyozuliwa. Haijuzu kusema kuwa Allaah hakumtuma Mtume Wake kwa mifumo iliyowekwa katika Shari´ah ambayo inaweza kuwafanya watenda madhambi wakatubia. Ni jambo linalotambulika vyema na kwa mapokezi mengi kwamba Allaah (Ta´ala) aliwasamehe makafiri wengi wasiohesabika kutokamana na ukafiri, ufuska na maasi kutokana na ile mifumo iliyowekwa katika Shari´ah ambayo haina hiyo mikusanyiko ya Bid´ahiliyotajwa. Bali wale wa awali waliotangulia, wale wahamaji na wanusuraji, na wale waliowafuata kwa wema, walitubu kwa Allaah (Ta´ala) kwa mifumo iliyowekwa katika Shari´ah na si kwa mifumo hii iliyozuliwa. Miji na vijiji vya waislamukatika nyakati zote imejaa watu waliotubu kwa Allaah na wakamcha Allaah na wakafanya yale mambo yanayopendwa na Allaah na kumfurahisha kwa kutumia njia zilizowekwa katika Shari´ah na si kwa njia hizi za Bid´ah.

Kwa hivyo haiwezekani kusema kwamba watenda maasi hawawezi kutubia isipokuwa kwa njia hizi za kizushi. Bali mtu anaweza kusema kuwa kuna Mashaykh ambao ni wajinga juu ya taratibu hizi zilizowekwa katika Shari´ah na zenye kuwashinda, hawana elimu ya Qur-aan na Sunnah na yale anayotakiwa kuwazungumzisha watu na kuwasikilizisha nayo katika yale ambayo Allaah hufanya akawasamehe kwayo, ambapo Shaykh huyu akapondoka kutokamana na njia zilizowekwa katika Shari´ah na badala yake akaziendea zile zilizozuliwa. Ima akafanya hivo kutokamana na nia njema – akiwa ni mtu wa dini – au ikawa lengo lake ni kutaka kuwa na utawala juu yao na kula mali zao kwa batili.

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/620-625)
  • Imechapishwa: 13/05/2024