Nitaamrisha vipi mema na kukataza maovu ilihali nina mapungufu tele?

Swali: Ikiwa mtu anahisi kuwa ana upungufu katika dini yake, je, aamrishe mema huku akiwa na upungufu na wakati mwingine anaogopa kujionyesha na hana elimu ya kutosha ya kufikisha ili aamrishe mema?

Jibu: Hakika shaytwaan hupenda sana kuwakatisha watu tamaa katika yale aliyowawajibishia Allaah ya kuamrisha mema na kukataza maovu kwa aina mbalimbali za shubuha na tafsiri. Mara humjia kwa kusema kwamba una upungufu na hujakamilika, basi vipi utaamrisha na kukataza! Mara humjia akisema kwamba naogopa usiwe ni mwenye kujionyesha kwa jambo hili. Yote haya ni katika vitimbi vya shaytwaan.

Sio sharti kwa mwenye kuamrisha na kukataza awe mkamilifu. Bali anatakiwa kuamrisha mema anayoyajua na kukataza maovu, hata kama ana upungufu au ana baadhi ya makosa. Lakini anatakiwa apambane na nafsi yake, amche Allaah na ajitahidi kutimiza aliyoyawajibisha Allaah na kuacha aliyoyaharamisha. Hata hivyo hilo lisimzuie kuamrisha na kukataza kwa elimu. Asiamrishe isipokuwa kwa ujuzi, kama alivyosema Allaah (´Azza wa Jall):

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi.”[1]

Akiona katika nyumba yake au kwa ndugu zake mtu anayepuuza swalah, hili ni jambo lililo wazi na halihitaji elimu nyingi. Swalah inajulikana kwa wote. Hivyo amuamrishe mema na amwambie amche Allaah, swali pamoja na waislamu na ihifadhi swalah. Afanye hivo kwa njia nzuri na kwa kumkumbusha adhabu ya Allaah na maradhi ya moyo. Adhabu kubwa zaidi ni moyo kufa. Adhabu kubwa ni moyo wa mtenda dhambi kufa. Matokeo yake asijue mema wala asikatae maovu na wala asijali kheri. Huenda akaathiriwa na ugonjwa khatari.

Kwa hiyo, ee ndugu, amrisha mema na kataza maovu hata kama una upungufu. Wala usiseme kuwa unaogopa kujionyesha, hapana. Amrisha mema, kataza maovu, fundisha kheri, lingania kheri na muombe Mola wako akupe afya njema. Jitahidi kuwa kumtakasia nia Allaah na pigana na mawazo ya kujionyesha yanayoweza kutokea. Yapinge hayo, azimia kuwa na kumtakasia nia Allaah na pata bishara njema ya kheri.

[1] 12:108

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3357/حكم-من-يامر-بالمعروف-وينهى-عن-المنكر-وعنده-تقصير
  • Imechapishwa: 23/09/2026