Swali: Baba yangu hasimamishi swalah msikitini wala nyumbani. Je, nikimwamrisha asimamishe swalah naye haswali ni lazima niondoke nyumbani au si lazima?

Jibu: Unapaswa kumshauri daima na ujitahidi katika kumshauri kwa mtindo mzuri na maneno mazuri. Haitakikani uondoke, kwa sababu kuwepo kwako kwake ni miongoni mwa sababu za kuongoka kwake. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema kuhusu wazazi washirikina:

وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا

“Wakikufanyia juhudi kwamba unishirikishe na yale usiyokuwa na elimu nayo, basi usiwatii. Lakini suhubiana nao kwa wema duniani.”[1]

Hivyo Allaah amemwamrisha mtoto wa wazazi washirikina atangamane nao duniani kwa wema. Hakumwamrisha awaache.

Kwa hiyo wewe tangamana naye duniani kwa wema kwa maneno mazuri na kumtimizia haja zake halali, chakula chake, kinywaji chake na mavazi yake. Umshauri daima na umuombee du´aa katika sujuud yako, mwisho wa swalah yako na kila wakati kwamba Allaah amuongoze, amneemeshe kwa uongofu na afungue moyo wake kwa imani. Wala usiondoke kwake. Bali tumia mitindo mizuri, maneno mazuri na upole. Huenda Allaah akamuongoza kupitia wewe. Kisha pia jitahidi kwa watu wema wanaomjua na kuwaheshimu ili waje kwake na wamshauri na wakusaidie katika sababu za uongofu.

[1] 31:15

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3372/كيفية-نصيحة-الاب-الذي-لم-يصل
  • Imechapishwa: 22/09/2026