Ni wajibu kufupisha swalah safarini

Swali: Kuna msafiri ambaye ilikuwa awaswalishe wakazi, akawaswalisha Dhuhr Rak´ah nne. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِذَا ضَرَبْتُمْ فِي الْأَرْضِ فَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَقْصُرُوا مِنَ الصَّلَاةِ

“Mtakaposafiri katika ardhi basi si dhambi kwenu kufupisha swalah.”[1]

Kitendo chake ameenda kinyume na Sunnah?

Jibu: Ndio, ameenda kinyume na Sunnah, kwa sababu haikuthibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikamilisha swalah safarini. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Makkah swalah ilifaradhishwa Rak´ah mbili. Baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhajiri al-Madiynah zikaongezwa Rak´ah zingine mbili isipokuwa Maghrib ambayo ni witiri ya leo na Fajr kwa sababu ya kisomo chake kirefu. Wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposafiri akaswali ile swalah ya mwanzo.”[2]

Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Swalah ya safari ni Rak´ah mbili. Zimeteremshwa kutoka mbinguni na yule mwenye kukataa anakufuru.”

Hili ni wajibu. Maoni sahihi ni kwamba ni wajibu kufupisha swalah. Sio ruhus peke yake, kama wanavosema Shaafi´iyyah. Wao wanaona kuwa kufupisha ni ruhusa na bora ni kuswali kikamilifu. Mambo sivyo hivyo. Ni lazima kufupisha kwa sababu haikuthibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali kikamilifu alipokuwa safarini.

[1] 04:101

[2] al-Bukhaariy na Muslim.

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Mu´aanid, uk. 297-298
  • Imechapishwa: 27/04/2025