Ni ipi hukumu ya kubadilisha mvi na ni kwa kitu gani mtu anabadilisha?

Swali: Ni ipi hukumu ya kubadilisha mvi na ni kwa kitu gani mtu anabadilisha?

Jibu: Kuzibadilisha nywele za mvi ni Sunnah iliyoamrishwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Zinaweza kubadilishwa kwa rangi yoyote isipokuwa tu nyeusi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza rangi nyeusi pale aliposema:

“… na jiepusheni na [rangi] nyeusi.”

Imepokelewa katika Hadiyth tishio kwa yule mwenye kuzipaka rangi nyeusi. Kwa hivyo ni wajibu kwa muumini ajiepushe kuzipaka rangi nyeusi kutokana na makatazo yanayopatikana ndani yake na makemeo kwa yule mwenye kufanya hivo. Jengine ni kwa sababu yule mwenye kupaka rangi nyeusi ni kama vile anapingana na desturi ya Allaah katika viumbe Wake. Hakika nywele katika hali ya ujana zinakuwa nyeusi. Zinapokuwa nyeupe kwa sababu ya uzee au sababu nyingine basi mtu anajaribu kukinzana na desturi hii na kutaka kuzifanya kama zilivyokuwa hapo kabla. Hapa kuna kitu katika kutaka kubadilisha uumbaji wa Allaah. Pamoja na haya yule mwenye kuzibadili kwa rangi nyeusi ni lazima imbainikie kuwa kweli amefanya hivo kwa sababu bado mizizi ya nywele itabaki kuwa mieupe. Mshairi amesema:

Tunazifanya nyeusi zile za juu na kukataa zile za chini

hakuna kheri katika matawi yanapokinzana na msingi

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/120-121)
  • Imechapishwa: 28/06/2017