Swali 1640: Je, inajuzu kupaka ndevu rangi nyeusi?

Jibu: Haijuzu kwa mwanaume kupaka ndevu zake rangi nyeusi, kwa sababu ya amri ya kuiepuka na katazo la kufanya hivo. Abu Daawuud amepokea kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah kwamba amesema:

“Abu Quhaafah aliletwa siku ya Ufunguzi wa mji wa Makkah, huku kichwa chake na ndevu zake zikiwa nyeupe kama mmea wa Thughaamah. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Badilisheni mvi hii na jiepusheni na rangi nyeusi.”[1]

Hadiyth hii ameipokea Muslim, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah.

Ahmad, Abu Daawuud na an-Nasaa’iy wamepokea kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kutakuwa na watu watakaopaka rangi nyeusi katika zama za mwisho, watakuwa kama vifua vya njiwa. Hawatanusa harufu ya Pepo.”[2]

Lakini inapendekezwa kubadilisha mvi kwa rangi isiyo nyeusi kwa mujibu wa Hadiyth iliyotajwa ya Jaabir.

[1] Ahmad (03/338), Muslim (06/155) na Abu Daawuud (4204).

[2] Ahmad (01/273) na Abu Daawuud (4212).

  • Muhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (5/166)
  • Imechapishwa: 23/10/2026