Nasaha kwa anayechelea kuhifadhi asije kusahau baadaye

Swali: Miongoni mwa utata ambao unanipitikia nafsini mwangu ni kwamba nikihifadhi Qur-aan nitasahau na vivyo hivyo nikihifadhi Hadiyth au venginevyo nitasahau na hivyo itakuwa ni hoja dhidi yangu. Kwa hivyo hakuna haja kwangu kuhifadhi. Ni vipi tutajibu utata huu?

Jibu: Yote haya yanatokana na shaytwaan. Mtu akijitahidi na akahifadhi yale atakayoweza basi haidhuru endapo atasahau. Kuhusu Hadiyth isemayo:

“Yule anayehifadhi Qur-aan kisha akaisahau basi atakutana na Allaah hali ya kuwa na ukoma.”

Ni Hadiyth dhaifu ambayo haikusihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwahi kusahau na akasema:

“Hakika mimi si venginevyo ni mtu ambaye nasahau kama mnavyosahau. Nikisahau basi nikumbusheni.”

Siku nyingine akasahau baadhi ya Aayah ambapo akasema:

“Allaah amrehemu fulani. Hakika amenikumbusha Aayah kadhaa na Aayah kadhaa. Zilikuwa zimenitoka.”

Hiki ni kitu ambacho hakina budi. Jambo hili ni katika maumbile ya mtu. Kwa hiyo mtu ajitahidi, asome na hifadhi kile kiasi atakachoweza kutoka katika Qur-aan na Hadiyth. Tukikadiria kuwa amesahau baadhi ya Aayah na baadhi ya Hadiyth haidhuru na hapana neno. Dunia ni nyumba ya mapambano. Ni lazima mtu apambane. Ahifadhi na kusahau kisha apambane kisha ahifadhi tena na kusahau. Ataendelea namna hiyo mpaka kithibiti.

Vivyo hivyo watu wengine kila ambaye amehifadhi Qur-aan ni lazima asahau sehemu. Lakini akijitahidi, akawa mkweli na akafanya subira kitathibiti.

Vivyo hivyo katika Hadiyth ahifadhi na kusahau, ahifadhi na kusahau. Akipambana kitathibiti au anlagau kwa uchache kitathibiti kingi chake.

Haikudhuru ukisahau kitu. Itakudhuru pale ambapo utapuuza, ukakengeuka na kughafilika. Lakini muda wa kuwa unapambana, unapupia na unajikumbusha kile ulichosahau hiyo ni jihaad kubwa katika njia ya Allaah. Isitoshe unapata thawabu nyingi katika jihaad hiyo.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://mufti.af.org.sa/ar/ftwa
  • Imechapishwa: 05/11/2022