Namna ya kutaamiliana na wafanyakazi wasiokuwa waislamu

Swali: Kazi yangu na aina ya majukumu yangu yanahitaji kukutana na jamii zisizo za Kiislamu na kuishi nao. Mara nyingine tunakula pamoja kazini. Huenda tukaanza kwa salamu au mamkizi. Je, tunawezaje kutekeleza jambo la kupenda na kuchukia kwa Allaah juu ya watu hawa?

Jibu: Unapaswa kuwanasihi na kuwalingania kwa Allaah na kutaamiliana nao kwa kadiri haja inavyopelekea. Ukiwauliza kuhusu kazi, ukawapa huduma inayohusiana na kazi na ukajibu pale wanapouliza, hapana vibaya. Ikiwa wameanza kutoa salamu,  unaitikia salamu. Lakini wewe usianze kuwatolea salamu. Ama kuwafanya ndio vipenzi na marafiki wa karibu na kuishi nao kana kwamba ni waislamu, hilo halifai. Lakini kuwatendea yale yanayohitajika Kishari´ah na kwa mujibu wa masharti ya kazi, hapana shida. Mfano kuuliza wameenda wapi, wametokea wapi, hali zao na hali ya watoto wao. Hili halihesabiwi kama kuanzisha salamu Wakianza kukutolea salamu, waitikie:

وعليكم السلام

”Nanyi amani iwe juu yenu.”

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/30094/كيف-يكون-الولاء-والبراء-مع-الزملاء-غير-المسلمين
  • Imechapishwa: 07/09/2025