Namna ya kujitwaharisha na janaba kwa asiyekuwa na maji

Swali: Tulienda na baadhi ya marafiki katika safari nje ya Riyaadh, khaswa Thumaamah. Tukaondoka usiku wa jumatano. Wakati wa kulala tulilala. Nilipoamka siku ya alkhamisi nikajikuta nimeota na nikawa na janaba. Tulikuwa wanne na hatukuwa na kitu isipokuwa galoni moja ya maji kwa kunywa na kula. Nikamweleza mmoja wa marafiki kuhusu jambo lililonipata ambapo akanambia nijitwahirishe kwa udongo na niswali pamoja nao Fajr na kwamba inafaa kufanya hivo. Nikafanya kama alivyonieleza. Lakini ulipofika wakati wa swalah ya Dhuhr nilianza kuwa na shaka katika jambo hili na hivyo sikuswali pamoja nao swalah zote kuanzia Fajr ya siku ya alkhamisi hadi ´Ishaa ya usiku wa ijumaa mchana. Tulipoenda Riyaadh niliziswali baada ya kuoga janaba, bila kufupisha swalah katika nyakati zote zilizopita. Ni nini kinanibidi katika hili?

Jibu: Ni wajibu kwako pale jambo kama hili likitokea uangalie. Ukiwa umepata maji karibu nawe ambayo unaweza kuoga kwa ajili ya janaba, basi yafaa na ni lazima uoge. Ikiwa hukupata, basi tafanya Tayammum kama alivyokuambia rafiki yako. Utajitwahirisha kwa udongo na itatosha. Kwa kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ

“Mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni na mkiwa wagonjwa au mko safarini au mmoja wenu akija kutoka msalani au mmewagusa wanawake kisha hamkupata maji, basi fanyeni Tayammum kwa ardhi kwa juu panguseni kwayo nyuso zenu na mikono yenu.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ardhi yote imefanywa kwangu ni sehemu ya kuswalia na ni kitu cha kutwahirisha. Basi yeyote katika ummah wangu pale utakapomfikia wakati wa swalah, basi mahali pake ndio msikiti wake na mahali pake pa kujitwahirisha.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Udongo umefanywa kwangu kuwa kitwahirisho ikiwa hatupati maji.”

Kwa hivyo asiyepata maji basi udongo ndio wudhuu´ wake. Basi ikiwa hukupata maji katika sehemu yoyote, unatakiwa kufanya Tayammum. Utapiga mikono yako ardhini, kisha utajipangusa usoni na viganja vyako, kama alivyoamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), kisha utaswali. Si lazima urudie tena swalah, kwa kuwa inatosha. Lakini ukiwa upo sehemu yenye maji, basi ni lazima uoge. Ikiwa wakati ni wa baridi, basi uyapashe maji kwa moto. Na kama hukupata moto na ukaogopa madhara ya baridi, basi unatakiwa kufanya Tayammum na kuswali na inatosha.

Ama kuacha kwako kuswali pamoja nao muda wote wa siku ya alkhamisi na ijumaa, hili ni kosa na ni makosa makubwa kwako. Ni wajibu kwako kutubia kwa Allaah kutokana na hilo, kujutia yaliyopita kwako na kutorudia tena. Umefanya jambo jambo jema kwa kuzilipa swalah wakati ulipopata maji. Lakini umefanya makosa kwa kuziacha na kwa kuchelewesha. Basi ni wajibu kutubia kwa hilo na kutozichelewesha swalah baada ya wakati wake. Ukiwa umepata maji, basi oga. Na usipopata, basi fanya Tayammum na uswali. Usizicheleweshe swalah nje ya wakati wake kamwe.

[1] 04:43

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/29985/ما-كيفية-الطهارة-من-الجنابة-عند-عدم-الماء
  • Imechapishwa: 01/09/2025