Namna hii inatakiwa iwe Khutbah ya ´iyd

Akimaliza swalah atatoa Khutbah mbili kwa kitako kimoja baina yake. ´Ubaydullaah bin ´Ubaydillaah bin ´Utbah amesema:

”Sunnah ni imamu katika ´iyd mbili atoe Khutbah mbili na atapambanua baina yake kwa kitako.”

Ameipokea ash-Shaafi´iy.

Ibn Maajah amepokea kupitia kwa Jaabir:

”Alitoa Khutbah hali ya kusimama, kisha akaketi chini kisha akasimama tena.”

Katika ”as-Swahiyh” na kwenginepo imekuja:

”Alianza kuswali, kisha akasimama hali ya kumwegemea Bilaal ambapo akaamrisha kumcha Allaah na akahimiza kumtii… ”

Kwa Muslim imekuja:

”Halafu anageuka hali ya kuwakabili watu kwa uso na huku watu wameketi katika safu zao.”

Katika ´Iyd-ul-Fitwr akiwahimiza watu kutoa Zakaat-ul-Fitwr na akiwabainishia hukumu zake kama mfano wa kiwango chake, wakati wake wa kuitoa na aina inayotolewa. Katika Khutbah ya ´Iyd-ul-Adhwhaa anawapendezea kuchinja Udhhiyah na kuwabainishia hukumu zake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika  ´Iyd-ul-Adhwhaa alibainisha hukumu zake nyingi.

Namna hii wahubiri wanatakiwa kutilia mkazo katika Khutbah zao kutegemea na minasaba. Wanatakiwa wawabainishie watu yale wanayoyahitajia katika kila wakati kutegemea na hali baada ya kuwausia juu ya kumcha Allaah, kuwawaidhi na kuwakumbusha. Namna hii khaswakhswa katika mikusanyiko mikubwa na minasaba mitukufu. Khutbah inapaswa iwe na yale mambo yanayowanufaisha wasikilizaji, amkumbushe mghafilikaji na amfunze mjinga.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mulakhaswsw-ul-Fiqh (01/274)
  • Imechapishwa: 29/07/2020