Swali: Je, inafaa kwa mwanamke kutoa katika mali zake peke yake swadaqah kwenda kwa mmoja katika ndugu ambaye kishakufa pasi na mume wake kujua? Ni ipi hukumu ikiwa swadaqah hiyo inatokamana na mali ya mume wake?

Jibu: Inafaa kwa mwanamke kutoa swadaqah kutoka katika mali zake mwenyewe kwenda kwa nduguze waliokufa akatoa kwa ajili ya kutafuta uso wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Thawabu na manufaa ya swadaqah hiyo itarudi kwao. Kwa sababu mwanamke huyo ana haki juu ya mali zake. Jengine ni kwamba yuko huru katika mali yake katika mipaka iliyowekwa na Allaah. Swadaqah ni kitendo chema ambacho thawabu zake zinarudi kwa yule aliyemtolea. Kwa hivyo hakuna ubaya kufanya hivo.

Ama kutoa swadaqah kutoka katika mali za mume wake ni jambo linahitajia upambanuzi; ikiwa mume wake ndiye kampa idhini au akatambua kuwa mumewe hatomzuia kufanya hivo na kwamba anapenda jambo hilo, basi atoe swadaqah kutoka katika mali zake katika yale mambo yaliyozoeleka kwa mujibu wa mila. Ama ikiwa mume wake alimkataza na hakumpa idhini, basi akomeke na asitoe kutoka katika mali zake hata kama atakuwa ni mwenye uwezo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (01/376)
  • Imechapishwa: 07/01/2020