Swali: Unasemaje kuhusu mwanamke na kulingania katika dini ya Allaah?

Jibu: Yeye ni kama mwanaume. Ni lazima kwake kulingania katika dini ya Allaah kwa kuamrisha mema na kukataza maovu. Kwa sababu maandiko kutoka katika Qur-aan tukufu na Sunnah zilizosafi zinafahamisha hivo. Maneno ya wanachuoni yako wazi katika hilo. Kwa hivyo ni lazima kwake kulingania kwa Allaah, kuamrisha mema na kukataza maovu kwa adabu za Kishari´ah zinazotakiwa pia kwa mwanaume. Ni lazima vilevile pamoja na hayo anapolingania kwa Allaah asihuzunike na asiwe na subira ndogo kwa sababu ya baadhi ya watu kumdharau, wakamtukana au wakamchezea shere. Bali ni lazima kwake kuwa na uvumilivu na subira ijapokuwa ataona kutoka kwa watu ambayo yanazingatiwa ni aina fulani ya uchezaji shere na kejeli. Kuna jambo lingine analotakiwa kulizingatia; anapaswa awe mfano mzuri inapokuja katika kujiheshimu, kujisitiri kwa Hijaab mbele ya wanaume ambao ni kando naye na ajiepushe kuchanganyikana na wanaume. Bali ulinganizi wake unatakiwa uambatane na kutilia umuhimu kujichunga na kila kile anachokikataza. Akiwalingania wanaume basi awalinganie ilihali amejisitiri pasi na kukaa faragha na yeyote katika wao. Akiwalingania wanawake awalinganie kwa hekima. Jengine anatakiwa awe msafi katika maadili na historia yake ili asije kupingwa na wakaanza kuulizana ni kwa nini asianze kwa nafsi yake mwenyewe. Ni lazima vilevile kujiepusha na mavazi ambayo yanaweza kuwatia mitihanini watu kwa sababu yake na aepuke sababu zote za fitina katika kuonyesha mapambo na kulegeza mazungumzo miongoni mwa mambo ambayo yeye mwenyewe anayakataza. Bali yeye mwenyewe anatakiwa kutiliwa umuhimu jambo la kulingania katika dini ya Allaah kwa njia ambayo haidhuru dini yake wala haidhuru sifa yake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/226) https://binbaz.org.sa/fatwas/875/%D8%A7%D9%84%D9%85%D8%B1%D8%A7%D8%A9-%D9%88%D8%A7%D9%84%D8%AF%D8%B9%D9%88%D8%A9-%D8%A7%D9%84%D9%89-%D8%A7%D9%84%D9%84%D9%87
  • Imechapishwa: 08/12/2019