Mwalimu na tabibu kupokea malipo kwa ajili ya kuwatibu watu

Swali: Mimi ni mwalimu wa kuhifadhisha Qur-aan Tukufu. Nimesikia baadhi ya watu wakisema kwamba haijuzu kuchukua malipo juu ya kufundisha Qur-aan na wala juu ya kuisoma. Je, hili ni sahihi au si sahihi?

Jibu: Sahihi ni kwamba inajuzu kuchukua malipo juu ya kufundisha Qur-aan, kufundisha Sunnah na tiba. Inajuzu kuchukua malipo juu ya hilo kwa yale yaliyothibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh kwamba kundi la Maswahabah walipita kwa kabila ambaye kiongozi wao alikuwa ameumwa (amepigwa na nyoka). Wakaja kwao watu wa huyo aliyeumwa, wakasema: ”Je, kuna miongoni mwenu anayetabana?” Wakasema: ”Ndiyo.” Wakasema: ”Hakika nyinyi hamkutukaribisha na hatutamfanyia matabano isipokuwa kwa malipo.” Wakakubaliana nao juu ya kundi la mbuzi. Mmoja katika Maswahabah akamfanyia matabano, akamsomea Suurah al-Faatihah na akaanza kumpulizia. Basi akasimama kana kwamba amefunguliwa kutoka kifungo na Allaah akamponya. Wakawapa malipo yao. Kwa hiyo Maswahabah wakasema kwamba hawatomtumia mpaka waende kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walipomjia na wakamwambia, akasema: “Mmefanya vizuri na nipeni sehemu pamoja nanyi.” ili kuwatuliza nafsi zao kwa hilo. Vilevile amesema:

“Hakika kilicho na haki zaidi kuchukua malipo juu yake ni Kitabu cha Allaah.”

Kwa hiyo mwalimu anapewa. Ikiwa hapewi, atafundishaje? Atajitoleaje kwa kufundisha? Anapewa mwalimu na mtabibu. Lakini kusoma tu kusoma? Hapana. Wanazuoni wameafikiana kwamba hapewi kwa kusoma tu. Kwa maana kwamba akaambiwa awasomee baadhi ya Aayah na watampa kadhaa, hili halijuzu, ambapo akasoma tu pekee. Ama elimu anayofundisha watu, anawaelekeza kwenye kheri, anawafundisha Qur-aan, anawafundisha Sunnah na anafundisha katika shule, anapewa mishahara ili ajitolee kwa jambo hili na ili achangamke katika hilo. Vivyo hivyo anatibu kwa Qur-aan, anatibu kwa du´aa, anafanya tiba ya Kishari´ah na tiba iliyoruhusiwa, anapewa malipo wake na hilo halina ubaya.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3477/هل-يجوز-اخذ-الاجرة-على-تعليم-القران-او-قراءته%C2%A0
  • Imechapishwa: 30/08/2026