Muhimu yawe manyonyesho matano II

Swali: Katika darsa iliyopita mlizungumza kuhusu kunyonya kunakowajibisha kwamba ni manyonyesho matano yenye kushibisha. Je, inawezekana kunyonyeshwa huko mara tano kukawa katika kikao kimoja cha dakika tano au kumi; kwa namna ambayo mtoto akashika titi kisha akaliachia kwa kutaka kwake mwenyewe, kisha akarudia tena kulishika, kisha akaliachia na vivyo hivyo mpaka atimize mara tano za kunyonya?

Jibu: Hapana, ni mara tano za kunyonyesha japo zisizo za kumshibisha. Sijasema “za kumshibisha”, Allaah akujaze kheri. Ni kunyonyesha japo zisizo za kumshibisha. Hakuna mwanachuoni yeyote aliyesema kuwa sharti ni “za kumshibisha”. Hapana, si lazima. Kunyonyesha kunatosha na kunaharamisha japo hakujamshibisha. Hivyo kushiba si sharti. Basi akinyonyeshwa mara tano, ni mamoja iwe katika kikao kimoja au vikao kadhaa, hata kama hakushiba, basi anakuwa ni mtoto wake. Kwa maana nyingine mtoto akinyonya, akanyonya titi na kumeza maziwa, na mama akawa na yakini na anajua kuwa amemeza maziwa, kisha akaachia titi, kisha akarudi tena akanyonya na kumeza maziwa, kisha akaachia, na vivyo hivyo mpaka atimize mara tano, ni mamoja iwe katika kikao kimoja, viwili au zaidi, basi anakuwa mtoto wake. Ni mara tano au zaidi, hata kama hakushiba, mradi ndani ya miaka miwili. Kwa hiyo ni lazima iwe kabla ya kuachishwa kunyonya.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/30082/ما-ضابط-الرضاع-الملزم-والمحرم
  • Imechapishwa: 06/09/2025