Swali: Imepokelewa katika Hadiyth Swahiyh kupitia kwa Mama yetu ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiamka asubuhi akiwa na janaba, kisha alikuwa akitawadha, akambusu mmoja wa wake zake na akaswali. Hali hiyo ilikuwa pia katika Ramadhaan.”

Swali ni ni kwamba: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angewezaje kuingia asubuhi akiwa na janaba, ilihali alikuwa ndiye imamu anayewaswalisha Muhaajiriin, Answaar na wengine waliyoingia katika Uislamu? Je, katika Hadiyth kuna dalili kwamba alikuwa akijamiiana baada ya swalah ya Fajr au alikuwa akiingiaje asubuhi akiwa na janaba? Je, busu halichengui wudhuu´? Kwa sababu tunawasikia baadhi ya wanazuoni wakisema kwamba busu ni miongoni mwa vinavyochengua wudhuu´. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwabusu wake zake baada ya wudhuu´ kisha anaswali bila kurudia wudhuu´. Tafadhali tufafanulieni hukumu ya suala hili kwa uwazi.

Jibu: Mosi ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijamiiana na baadhi ya wake zake wakati wa usiku, kisha wakati mwingine hakuoga usiku na hivyo akiamka asubuhi akiwa na janaba, kisha akaoga kwa ajili ya swalah ya asubuhi.

Pili ni kwamba busu halichengui wudhuu´ kwa maoni sahihi ya wanazuoni, hata ikiwa mtu atapata ladha ya jambo hilo, muda wa kuwa hakutokwa na manii. Pia busu halivunji swawm.

  • Muhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (5/269)
  • Imechapishwa: 09/11/2026