Mtu anafanya nini na pesa ya ribaa?

Swali: Nina baba yangu ambaye amekuwa akifanya kazi katika kampuni ya Aramco kwa muda wa miaka 33. Tangu alianza kazi alikuwa akiweka pesa zake katika benki ya hifadhi ya kijamii ya kampuni. Sasa amemaliza kazi na watampa pesa zake pamoja na nyongeza au mara dufu yake. Sasa afanye nini kwa pesa hizi? Je, ni ribaa? Mimi nifanye nini iwapo atazipokea?

Jibu: Kuhusu jambo hili imetolewa fatwa na kamati ya kudumu kwamba pesa zinazowekwa katika kampuni ambazo zinashurutisha mfanyakazi kutoa sehemu ya mshahara wake kila mwezi, kisha baada ya miaka mitano kumpa kiasi fulani na baada ya miaka kumi kumpa asilimia fulani kama asilimia 60, 50 au 100, basi nyongeza hii ni ribaa. Kwa sababu wao wananufaika na pesa zake, wanazizidisha na kufanya biashara ya ribaa, kisha wanawapa wafanyakazi hiyo faida. Hili tumeliona katika baadhi ya masharti ya kampuni, kwamba baada ya kupita miaka mitano wanakupa asilimia 50, zaidi au pungufu, na baada ya miaka kumi wanakupa asilimia 100 kutokana na makato uliyoweka, jambo ambalo ni ribaa.

Kinachotudhihirikia ni kwamba wajibu ni kuzigawa pesa hizo kwa njia ya swadaqah au kuzitoa katika miradi ya kheri. Asizile kwa sababu ni ribaa. Achukue tu mali yake aliyokusanya kutokana na makato yake aliyolipa. Ama ribaa waliyompa kama nyongeza, hii itolewe katika mambo ya kheri na kazi za heri kama kujenga barabara, shule, vyoo, kusaidia masikini, kulipa madeni ya waliodaiwa, kuwasaidia Mujaahiduun na wenye matatizo ya umasikini popote pale. Hili ndilo lililo wajibu, kwa sababu ni mali iliyomjia si kwa njia halali, basi haichomwi wala kuharibiwa. Badala yake inatolewa katika matumizi ya mali zisizo na mmiliki au zisizokuwa halali kumilikiwa.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/29992/اين-تصرف-اموال-الربا-وهل-يحل-تملكها
  • Imechapishwa: 03/09/2025