Mswaliji ametambua katikati ya swalah kuwa imamu hana wudhuu´

Swali: Kuna mswaliji aliswali nyuma ya imamu ambaye akaona kwenye unyayo wa imamu sehemu ndogo ambayo haikufikiwa na maji.  Mswaliji huyu afanye nini ilihali anaswali nyuma ya imamu huyo na yeye ndio ameshaona weupe huo?

Jibu: Anuie kujitenga naye na pindi atapomaliza kuswali amweleze. Kuhusu wale maamuma ambao hawakutambua hilo swalah zao ni sahihi. Ama huyu mswaliji huyu anatakiwa kujitenga na kukamilisha swalah yake peke yake. Kwa sababu hivi sasa anaswali nyuma ya imamu ambaye anaamini kuwa swalah yake ni batili kwa kuwa hakutawadha. Kwa hivyo ajienge na atoe Tasliym. Pindi imamu atapomaliza swalah yake amzindue. Ni wajibu kwa imamu kurudi kutawadha na kuswali upya. Kuhusu maamuma hawana juu yao kitu.

Hii ni kanuni yenye faida ambayo nawapa: imamu akiswali hali ya kuwa hana wudhuu´ na asitambue hilo isipokuwa baada ya kumaliza kuswali, basi anachotakiwa ni yeye kurudi kutawadha na kuswali tena. Maamuma hakuna kinachowalazimu. Endapo atajua hilo katikati ya swalah, anatakiwa kutoka nje ya swalah na awaambie waswaliji: “Ee fulani! Watimizie swalah yao.” Ikiwa kumebaki Rak´ah moja watatakiwa kuswali ngapi? Rak´ah moja. Kwa hivyo atawakamilishia swalah yao. Asiposema hivo, basi anatakiwa kumtanguliza mbele mmoja wao. Asipofanya hivo, basi kila mmoja anatakiwa kukamilisha swalah kivyake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (40) http://binothaimeen.net/content/900
  • Imechapishwa: 22/08/2018