Allaah ameamrisha umoja na kuungana na akakataza kufarikiana na tofauti. Kwa ajili hiyo Allaah ameamrisha sababu zote zinazopelekea katika ugomvi, chuki na mfarakano na badala yake akaamrisha sababu zote zinazopelekea katika kuungana na kupendana. Amekokoteza kuleta upatanishi na akafanya ni katika matendo bora kabisa. Vilevile ameamrisha kulazimiana na mkusanyiko na akakhabarisha (Subhaanah) kupitia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba mkono Wake uko pamoja na mkusanyiko. Amemwamrisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuswali nyuma ya viongozi. Ni mamoja wakawa wema au waovu midhali uovu wao haujawatoa katika Uislamu. Pia ameamrisha kupigana Jihaad bega kwa bega pamoja na viongozi na akaeleza kuwa Jihaad na Hajj itakuwa ni yenye kuendelea pamoja nao mpaka pale Qiyaamah kitaposimama. Sambamba na hilo amekataza kuwafanyia uasi na mtu kujivua katika utiifu wao. Yote haya ni kwa sababu ya yale manufaa yanayopatikana katika umoja na kufungamana ambako natija yake inarudi katika Uislamu na waislamu katika kupatikana nguvu na mafungamano.

Msingi huu ni moja katika misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah iliyoandikwa katika vitabu vya ´Aqiydah ili uwe ni msingi miongoni mwa misingi ya Uislamu. Hawakuitwa ´ Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah` isipokuwa ni kwa sababu ya kuchunga msingi huu mkubwa ambao wameteleza kwao Ahl-ul-Bid´ah wadh-Dhwalaal wengi. at-Twahaawiy amesema katika “´Aqiydah” yake:

“Tunaona kuwa mkusanyiko ni haki na ni sawa. Vilevile tunaona kuwa kufarikiana ni kupinda na adhabu.”

Tunachotaka kusema ni kuwa kufarikiana ni kupinda kutoka katika njia. Kwa ajili hii utawaona walinganizi waliopinda wanalingania kutoka katika mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ambao wao wanaamrisha umoja.

Kinachosikitisha ni kuwa al-Hajuuriy amepuuzia msingi huu. Amewapuuza Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wote isipokuwa tu wale wanaokubaliana naye. Amewafanyia Tabdiy´ watu wasiokuwa na hatia na akawahukumu upotofu kwa dhuluma, unyanyasaji na uadui. Hakuna jambo khatari kabisa katika mfarakano kama hilo. Atakayefuata mfumo wa wanachuoni basi ataona aibu kufanya unyanyasaji kama huu na hukumu hizi za kijasiri zitamrudilia yeye mwenyewe na badala yake yeye ndiye atayetoka katika mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

  • Mhusika: Shaykh Abu ´Ammaar ´Aliy al-Hudhayfiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://m-noor.com/showthread.php?p=33728
  • Imechapishwa: 14/01/2017