Msafiri amfuate imamu wake mkazi

Swali: Wakati msafiri alipoingia msikitini na akawakuta watu wanaswali Dhuhr, akamwacha imamu kwanza aswali Rak´ah mbili kisha baadaye ndio akajiunga na imamu katika zile Rak´ah mbili za mwisho. Je, kitendo chake ni sahihi au si sahihi?

Jibu: Si sahihi. Ni wajibu kwake kuswali swalah ya imamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msikhitilafiane na maimamu wenu.”

“Hakika mambo yalivyo imamu amewekwa ili afuatwe.”[1]

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) alipoambiwa kwamba baadhi ya watu wanaswali Rak´ah nne pamoja na imamu katika Haram na Rak´ah mbili wanapokuwa kwenye mahema yao huko Abtah, akasema:

“Hiyo ndio Sunnah ya Mtume wenu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Kwa hivyo maoni sahihi ni kwamba ni wajibu kumfuata imamu. Imamu akiswali Rak´ah nne, basi naye aswali Rak´ah nne. Msafiri amfuate imamu wake ambaye ni mkazi. Akiona kuwa imamu wake amekosea ataswali Rak´ah mbili na kumaliza kwa Sujuud mbili za kusahau.

[1] al-Bukhaariy (688) na Muslim (412).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Mu´aanid, uk. 298-299
  • Imechapishwa: 27/04/2025