Mposaji ameshurutishwa na baba mkwe kumtaliki mke wake wa kwanza

Swali: Je, wale ambao mwanamume anataka kuwaoa wanaruhusiwa kumwekea sharti kwamba amtaliki mke wake wa kwanza? Je, inajuzu kwake kukubali sharti hilo bila sababu yoyote kutoka kwa huyo mke wa kwanza?

Jibu: Hili halijuzu. Baadhi ya watu wakitaka kuozeshwa, wakija mtu kuwaomba msichana wao naye ana mke, wao humuwekea sharti kwamba amtaliki mke wake. Haya hayafai. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza jambo hili. Amekataza mwanamke kumwekea sharti mwenzie kuachwa. Kwa hiyo haijuzu kwa wanaotolewa posa kumlazimisha mchumba amwache mke wake wa sasa. Hilo ni dhuluma na uonevu. Hawana haki ya sharti hilo. Pia yeye halazimiki kulitimiza, kwa sababu ni sharti batili. Awaambie kuwa jambo hili halijuzu na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amelikataza na halifai kutamkwa sharti kama hilo. Wakisisitiza, basi sharti lao ni batili, kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kisa cha Bariyrah:

“Kila sharti lisilokuwa ndani ya Kitabu cha Allaah ni batili, hata kama ni masharti mia. Hukumu ya Allaah ndiyo yenye haki zaidi na sharti la Allaah ndilo imara zaidi.”

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1249/حكم-اشتراط-الزوجة-الثانية-طلاق-الزوجة-الاولى
  • Imechapishwa: 13/02/2026