Mke ana wivu unaosababisha hapa na hapa kugombana na mume wake

Swali: Siku zote kunatokea ugomvi kati yangu mimi na mume wangu kwa sababu ya wivu wangu juu yake. Mimi nina wivu nae na nachunga mitazamo yake. Anapotoa mtazamo wowote au nikamshakia basi huwa na wivu juu yake. Siku zote hutumia hoja dhidi yangu kwamba wivu wenye kusifiwa kwa Allaah ni mtu kuwa na wivu juu ya yale Allaah aliyokataza. Ama kuhusu wivu unaotoka kwangu hausababishi jengine isipokuwa tu talaka. Mimi sikufurahishwa na maneno yake kwa kuwa naamini miongoni mwa haki zangu ni mimi kuwa na wivu juu yake hata kama hakukusudia. Hata hivyo ni mwanaume mwenye msimamo na sina mashaka nae. Naomba nasaha vile unavyoonelea.

Jibu: Namnasihi mwanamke huyu apunguze wivu wake. Vinginevyo wivu ni katika maumbile ya mwanamke. Mwanamke anakuwa na wivu kwa mume wake. Hii ni alama kwamba anampenda. Lakini nasema kwamba wivu ukizidi sana basi huwa na maradhi. Sivyo tu bali unakuwa sasa ni wenye kumpa tabu mwanamke. Tabu kwelikweli. Kwa hivyo mimi namshauri mwanamke huyu kupunguza wivu wake. Vilevile namshauri mwanaume pia amshukuru Allaah (´Azza wa Jall) kumpa mwanamke mwema na anayempenda. Kwa sababu wanandoa kupendana ni miongoni mwa mambo yanayofanya maisha yao kuwa na furaha. Vinginevyo wivu ni jambo la kimaumbile ambalo halina budi.

Kuna mmoja katika wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtumia chakula Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kilichokuwa ndani ya chombo wakati ambapo ilikuwa ni zamu ya mke wake mwengine. Pindi mjumbe alipoingia akiwa na chakula kilichokuwa ndani ya chombo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakifurahikia. Mjumbe yule akampatia nacho Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilihali ilikuwa ni zamu ya mwanamke mwengine. Mwanamke huyu ambaye ilikuwa ni zamu yake akaona wivu. Akaupiga mkono wa Mtume, akachukua kile chombo na kukivunja na chakula kikasambaratika. Lakini hata hivyo Mtume hakumkaripia. Alichosema ni:

“Mama yako ameona wivu.”

Au alisema maneno kama hayo. Akaokota kile chakula na chombo na akachukua chakula cha yule mwanamke ambaye alikuwa nyumbani mwake na chombo chake ambapo akasema:

“Chombo kwa chombo na chakula kwa chakula.”

Akamuagiza yule mjumbe. Alifanya hivi kwa sababu yule mjumbe ataporudi alikotoka na kumueleza alichofanya yule mwanamke mwengine atamuona vibaya. Lakini chombo kikija kimeharibiwa na chakula kimeharibiwa ataingiwa na baridi. Hii ni hekima ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tunachotaka kusema ni kwamba wanawake kuwa na wivu ni kitu cha lazima.

Naona kuwa miongoni mwa neema za Allaah kwa mume ni mke awe mwenye kumpenda kufikia katika kiwango hichi. Lakini hata hivyo namshauri mwanamke huyu apunguze wivu wake ili usije kukutaabisha bure.

Pia namshauri mwanaume amshukuru Mola wake juu ya neema hii na wala hilo lisikuzidishie jengine isipokuwa kuzidi kumpenda mke wako.

Ama kuhusu masuala ya talaka usiyataje hata siku moja kumtajia mke wako. Pindi mwanaume anapomtajia talaka mwanamke basi inakuwa ni kama kinyago mbele ya macho yake sawa anapokuwa amelala au macho. Kwa ajili hii ni katika upumbavu kuona baadhi ya watu wanawatajia wanawake neno ´talaka`. Haifai kufanya hivo hata kama ni kwa lengo la kutaka kumtisha. Tisha kwa kitu kingine kisichokuwa hichi. Kutishia kwa talaka matokeo yake shaytwaan hutendea kazi polepole moyoni mwake mpaka hatimaye mwishoni kunatokea kutengana.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (31) http://binothaimeen.net/content/708
  • Imechapishwa: 03/11/2017