Mimba ambayo madaktari wamethibitisha mtoto ana kasoro ya kimaumbile

Swali: Madaktari wakithibitisha kuwa mtoto huyu ni mwenye umbile la muumbuko tumboni mwa mama yake na daktari akaashiria kuiangusha mimba hii na mama yake akakubaliana na hilo na wakamwambia kuwa wataiangusha kwa kutumia miale. Ni ipi hukumu ya kuiporomosha? Ni zipi hukumu zinazopelekea juu ya hilo?

Jibu: Ikiwa kipomoko hicho kimeshapuliziwa roho – jambo ambalo hufanyika pale anapotimiza miezi mine – basi itambulike kuwa hichi hakijuzu kukiangusha kwa hali yoyote ile. Ni mamoja kina muumbuko au kubaki kwake mpaka wakati wa kujifungua kitamsababishia mama kufikwa na maradhi au hata kuangamia. Kwa hali yoyote haijuzu kuiporomosha kabisa. Haijalishi kitu hata kama madaktari watathibitisha kwamba endapo mimba hiyo itabaki tumboni mwake basi atakufa, tunasema afe na hawezi kuiporomosha. Kwa nini? Kwa sababu tukikusudia kumuua ni kuiua nafsi pasi na haki. Hiki ni kipomoko ambacho hakikutenda jinai na hakikumshambulia mtu. Kwa nini tukiue? Mtu akisema kwamba akiachwa tumboni mwa mama yake basi si mama yake wala mtoto huyo wote wawili watakufa. Hili tunalijibu kwa njia mbili:

1- Mama yake akifa na ikawa ni katika muda ambao bado anaweza kuwa yuhai, basi watu wanaweza kukimbilia kumfanyia upasuaji na wakampasua tumbo lake hata kama ni baada ya kufa na mtoto huyo akatolewa. Hili ni mosi.

2- Tukikadiria kuwa hili haliwezekani na kwamba haiwezekani kumtoa mtoto na kwamba kubaki kwake itakuwa ni sababu ya kufa kwa mama yake, tunauliza akifa mama yake amekufa kwa sababu yetu sisi au ni kwa sababu Allaah ametaka? Ni Allaah. Sisi hatuna uwezo. Lakini endapo sisi tutamtoa mtoto na akawa amekufa, basi sisi ndiye tumesababisha. Hapa ni pale ikiwa tayari ameshapuliziwa roho na ni baada ya kutimiza miezi mine.

Ama ikiwa ni kabla ya hapo, jambo ni jepesi kiasi. Mimba hiyo inaweza kutolewa na kuporomoshwa. Kwa sababu hivi sasa hajauwa mtu ambaye amepuliziwa roho. Kwa ajili hii Allaah (´Azza wa Jall) amesema wakati alipokuwa anaelezea ukuaji wa kipomoko:

ثُمَّ أَنشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ

“Kisha Tukamuanzisha kiumbe kingine.”[1]

Ametoka katika kitu kisichokuwa na uhai na kwenda katika uhai.

Kujengea juu ya hili tunasema, hayo ikiwa yatafanyika baada ya kutimiza miezi mine – nao ni ule wakati baada ya kupuliziwa roho – basi kuiangusha ni haramu hata kama kubaki kwake kutapelekea kufa kwa mama yake. Hili ni mosi. Ikiwa ni kabla ya hapo hakuna neno. Ikiwa madaktari watathibitisha kuwa atatoka hali ya kuumbuka na atachoka yeye na kuwachosha familia yake au wakasema kuwa kubaki kwake itakuwa ni sababu ya kufa kwa mama yake, basi katika hali hiyo hakuna neno kuitoa mimba hiyo.

[1] 23:14

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (38) http://binothaimeen.net/content/871
  • Imechapishwa: 18/06/2020