Swali: Imepokelewa ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpa ruhusa ya kubusu mzee na akamkataza kijana. Je, Hadiyth hii ni Swahiyh?

Jibu: Hili linahusu swawm, swawm ya Ramadhaafn. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anabusu huku akiwa amefunga na alikuwa anafanya mambo ya kimapenzi huku akiwa amefung. Kwa hiyo aliyefunga ana ruhusa ya kumbusu mke wake na kufanya naye mambo ya kimapenzi akiwa amefunga ikiwa anajiamini kutotumbukia kwenye machafu na ikiwa matamanio yake si ya haraka na haimdhuru jambo hilo, basi katika hali hiyo hapana vibaya. Ama yule ambaye matamanio yake ni ya haraka – akibusu hutokwa manii au anaogopa kuingia kwenye jimaa – basi ajiepushe na hilo. Imepokewa kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimruhusu bwana mmoja katika kubusu na akamkataza bwana mwingine. Akatazama katika hilo akakuta aliyeruhusiwa ni mzee na aliyekatazwa ni kijana. Hii kama ingesihi, kuna udhaifu katika cheni ya wapokezi wake. Ameipokea Abu Daawuud na katika cheni ya wapokezi wake kuna udhaifu. Lakini hata kama imesihi, maana yake ni kuwa mzee kwa kawaida huwa dhaifu katika matamanio na kijana huwa na matamanio mengi na nguvu zaidi. Kwa hiyo akakatazwa kufanya mambo ya kimapenzi kwa sababu ya nguvu ya shahwa yake. Hata hivyo Hadiyth hiyo ni dhaifu. Hadiyth Swahiyh zinafahamisha kufaa kwa jambo hili kwa wote wawili; kijana na mzee. Hadiyth Swahiyh zinajulisha kufaa kufanya mambo ya kimapenzi na kumbusu mke katika hali ya swawm kwa kijana na mzee kwa pamoja, isipokuwa kwa yule ambaye shahwa yake ni kali na anaogopa shari ya uchafu. Katika hali hiyo huyu aache jambo hilo, hata kama ni mzee. Baadhi ya wazee wana matamanio makali zaidi kuliko vijana wengine.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1216//fatwas/1216/الحكم-على-حديث-رخص-بالقبلة-لشيخ-ونهى-عنها-شابا
  • Imechapishwa: 26/02/2026