Swali: Mama yangu amefariki na nataka kumzawadia thawabu zangu. Je, nimuombee du´aa, nimsomee Qur-aan, nimtolee swadaqah au nimsomee al-Faatihah?

Jibu: Mtolee swadaqah. Bwana mmoja alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mama yangu amekufa. Nadhani kuwa lau angeliweza kutamka basi angetoa swadaqah. Je, nimtolee swadaqah?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ndio.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapofariki mwanadamu basi matendo yake hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu ambayo watu wananufaika nayo au mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa.”[2]

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amepokea kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba kuna mwanamke alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama anatakiwa kulipa siku za mama yake za Ramadhaan? Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akajibu:

“Unaonaje lau mama yako angelikuwa na deni ungelimlipia nalo? Deni la Allaah lina haki zaidi kulipwa.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayekufa na ameacha swawm anayodaiwa, basi atafungiwa na walii wake.”[4]

Kuhusu kumsomea Qur-aan, kukiwemo al-Faatihah, ni jambo halikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wala kisomo hakimfikii, kwa sababu Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ

“… mtu hatopata [malipo] isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi… ”[5]

Aayah ni yenye kuenea na haifanywi kuwa ni maalum isipokuwa kwa dalili maalum.

[1] al-Bukhaariy (2670) na Muslim (1004).

[2] Muslim (1631).

[3] Ahmad (2005) na Abu Daawuud (3310). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (2831). Hadiyth kama hiyo inapatikana katika al-Bukhaariy (1953) na Muslim (1148) tofauti muulizaji ni mwanaume.

[4] al-Bukhaariy (1952) na Muslim (1147).

[5] 53:39

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Mu´aanid, uk. 216-217
  • Imechapishwa: 03/08/2025