Maoni mafupi ya al-Albaaniy juu ya Jamaa´at-ut-Tabliygh

Swali: Unasemaje juu ya Jamaa´at-ut-Tabliygh? Je, unapendekeza kutoka pamoja nao? Wanazuoni na wanafunzi wana jukumu gani juu yao?

Jibu: Nimetaja mara nyingi maoni yangu kuhusu Jamaa´at-ut-Tabliygh. Kwa kufupisha ni kwamba kundi kama kundi wanaweza kukusudia kheri, lakini kheri haipatikani isipokuwa katika njia aliyokuja nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kutoka kwa sampuli hii ni Bid´ah ya kisasa. Hawaitambui wanazuoni wa waislamu kuanzia wale wa kale mpaka wa sasa. Wanajengea hoja baadhi ya Hadiyth ambazo ukweli wa mambo ziko dhidi yao na haziwasapoti. Kwa ajili hiyo sisi tuliwanasihi, na bado tunaendelea kuwanasihi, watoke kwa ajili ya kujifunza na kusoma elimu na waketi misikitini katika duara za kielimu, wasome na kuifahamu Qur-aan. Aidha wanatakiwa vilevile kujifunza elimu ya Hadiyth na kuzifahamu. Wamepewa mazoezi ya kufanya ujasiri wa kusimama na kutoa Khutbah, kutoa mawaidha na nasaha ilihali hawawezi hata kusoma Aayah moja ndani ya Qur-aan kama ilivyoshushwa.

Kile ninachoona ikiwa wataridhia kuamrisha mema na kukataza maovu basi kutoka pamoja nao itakuwa ni njia ya lazima ya kuwalingania wale wenye haja na ulinganizi huo. Lakini tunachokijua kutoka katika miji mingi ya kiarabu, sembuse miji isiyokuwa ya kiarabu, ni kwamba hawamwachi mtoa nasaha awanasihi wala alinganie katika Qur-aan na Sunnah ikiwa sio katika ule wigo ambao wao wenyewe wamejiwekea. Inahusiana na mfumo wenye kubana mno ambao unapingana na maandiko ya Shari´ah ambayo yanawaamrisha kwa uchache kundi la watu kusimamia jambo la kuamrisha mema na kukataza maovu. Haya ndio maoni yangu kwa ufupi juu ya kundi hili. Nimewazungumzia mara nyingi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Juddah (26 A)
  • Imechapishwa: 13/05/2022