Manii kutoka kwa matamanio kwa mfungaji mwenyewe kusababisha ni jambo linaiharibu swawm kwa mujibu wa maimamu wanne; Maalik, Abu Haniyfah, ash-Shaafi´iy na Ahmad.

Ama kuhusu madhiy kutoka kwa matamanio, hakuiharibu swawm. Haiwezekani ikawekwa katika hukumu moja na manii. Kwa kuwa madhiy hayawajibishi kuoga na sio matamanio. Kwa ajili hii yanamtoka mtu pasi na kupata hisia tofauti na manii. Kwa ajili hii si sahihi kuyaweka katika mkumbo mmoja na manii. Msingi ni kubaki kwa swawm na kusihi kwake mpaka kusimame dalili [ya wazi] juu ya kuharibika kwake. Kanuni hii inatakikana kwa mwanafunzi aihifadhi. Kila kilichothibiti katika Shari´ah, hakivunjiki isipokuwa kwa Shari´ah, bi maana kilichothibiti kwa dalili ya Kishari´ah hakitenguki isipokuwa kwa dalili ya Kishari´ah. Swawm hii ikithibiti haiwezi kuharibika isipokuwa kwa dalili kutoka katika Shari´ah. Hakuna dalili inayoonesha kuwa madhiy yanaiharibu swawm. Hii pia ndio kauli ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah). Vilevile ndio madhehebu ya adh-Dhwaahiriyyah na hata hivyo ni sahihi. Yamekuwa mambo mangapi ambayo tumeshataja?

1- Kula.

2- Kunywa.

3- Jimaa.

4- Kujitapikisha kwa makusudi.

5- Kutoa damu kwa kufanya Hijaamah.

6- Kutoka damu ya hedhi.

7- Kutoka kwa damu ya nifasi.

8- Vitu ambavyo vina maana ya kula na kunywa.

9- Mfungaji kujitoa manii kwa matamanio.

Mambo haya yanayoiharibu swawm yana kafara? Jibu ni hapana. Hakuna kilicho na kafara ispokuwa moja katika hayo, nacho ni jimaa. Jimaa ina kafara. Kwa sharti iwe katika mchana wa Ramadhaan miongoni mwa wale ambao swawm inawawajibikia. Ikiwa ni nje ya mchana wa Ramadhaan, kwa mfano mtu analipa siku zake za Ramadhaan [alizokula] kukatokea jimaa, hana juu yake kafara. Ikiwa ni katika mchana wa Ramadhaan miongoni mwa wale amabao swawm haiwawajibikii, kadhalika hana juu yake kafara. Kwa mfano mwanaume awe katika safari na mke wake na wote wawili wamefunga, lakini wakati wa mchana akamwingilia mke wake, atakuwa hana juu yake kafara kama jinsi hapati madhambi pia. Kwa kuwa msafiri inajuzu kwake kukata swawm yake kwa kitu chochote miongoni mwa vile Alivyovihalalisha Allaah (´Azza wa Jall). Hivyo basi, ni kipi kinachomlazimu? Kulipa kwa sababu amekata swawm yake. Ni lazima kwake kulipa.

Isitoshe ni kwamba, mambo haya yanayoharibu swawm hayaiharibu isipokuwa mtu akiyafanya kwa ujuzi, mwenye kukumbuka na hali ya kuwa ni mwenye kukusudia. Kuwa ni mjuzi kinyume chake ni kutokujua. Kukumbuka kinyume chake ni kusahau. Kukusudia kinyume chake ni kutokukusudia. Lau kwa mfano mtu atakula na kunywa akifikiria kuwa alfajiri haijaingia, kisha ikabainika kuwa kumeshapambazuka, hana juu yake kulipa na swawm yake ni sahihi kwa kuwa hakujua. Lau atakula kwa kusahau, swawm yake ni sahihi. Lau atakula kwa kutenzwa nguvu, bi maana amekuja mtu na kumtisha kumuua na kipigo cha kuumiza na hilo likamfanya kula, hana juu yake kulipa na swawm yake ni sahihi. Kadhalika lau atasukutua na maji yakaingia kwenye koo yake bila ya kukusudia, swawm yake ni sahihi kwa kuwa hakufanya kwa kukusudia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kanda “Liqaa´aatu Ramadhwaaniyyah”, sehemu ya 01
  • Imechapishwa: 23/09/2020