Sijui dalili yoyote ya kufanya ´ibaadah maalum katika Rajab. Yale yanayofanywa kwa mnasaba wa Rajab yanazingatiwa ni Bid´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote anayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu, atarudishiwa mwenyewe.”[1]

Zipo Bid´ah zingine zinazofanywa katika Rajab. Wanawake huku kwetu wanaimba na kusifu mwezi kama sikukuu ya sherehe na ijumaa yake ya mwezi. Vivyo hivyo kuhusu Bid´ah inayohusiana na usherekeaji wa Safari ya usiku na ya Kupandishwa juu ya mbinguni, usiku wa tarehe 27 Rajab. Tarehe ya Safari ya usiku na ya kupandishwa mbinguni haikuthibiti kabisa, kama ilivyo katika “Tabiyiyn-ul-´Ajab fiy Fadhwli Rajab”. Wale wanaotoa pesa zao katika minasaba hii wataulizwa juu yake mbele ya Allaah. Abu Barzah al-Aslamiy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Haitovuka miguu ya mja siku ya Qiyaamah mpaka aulizwe juu ya mambo mane: umri wake aliuteketeza katika mambo gani, elimu yake aliifanyia nini, mali yake aliipata kivipi na akaitumia wapi na mwili wake aliutumia vipi?”[2]

Vivyo hivyo kuhusu wakati wake na mwili wake anaotumia katika usiku huo. Bid´ah za Suufiyyah zimeushambulia Uislamu na zimewatengenezea njia wakomunisti na vyama vyengine. Ni haramu kwa muislamu kuhudhuria Bid´ah hizi. Kwani haijuzu kwake kuongeza idadi ya Ahl-ul-Bid´ah. Ni haramu kwa muislamu kushirikiana nao katika mambo haya. Mwenye kufanya hivo anashirikiana nao katika batili na kuwatia nguvu katika batili. Uhakika wa mambo ni kwamba waislamu wanapaswa kuwakemea mambo hayo. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ ۚوَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Wawepo kutoka kwenu watu wanaolingania kheri na kuamrisha mema na unaokataza maovu. Hao ndio waliofaulu.”[3]

لُعِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَىٰ لِسَانِ دَاوُودَ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ ۚ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوا وَّكَانُوا يَعْتَدُونَ كَانُوا لَا يَتَنَاهَوْنَ عَن مُّنكَرٍ فَعَلُوهُ ۚ لَبِئْسَ مَا كَانُوا يَفْعَلُونَ

“Wamelaaniwa wale waliokufuru miongoni mwa wana wa israaiyl kupitia ulimi ya Daawuud na ‘Iysaa mwana wa Maryam – hivyo ni kwa sababu ya kuasi kwao na walikuwa wakivuka mipaka. Walikuwa hawakatazani maovu waliyofanya!”[4]

Ni wajibu kuwakemea, sembuse kuhudhuria na kubariki vikao vyao vilivyozuliwa vinavyowakimbiza watu mbali na Allaah. Muislamu hazushi Bid´ah yoyote isipokuwa huacha Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mfano wake.

[1] Muslim (1718).

[2] Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (1/162).

[3] 3:104

[4] 5:78-79

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Mu´aanid, uk. 292-293
  • Imechapishwa: 04/08/2025