Swali: Ni ipi hukumu ya kuswali juu ya magazeti yanayoenea siku hizi?

Jibu: Haijuzu kuswalia juu ya magazeti, kwa sababu yana utajo wa Allaah, yana Hadiyth na Aayah. Kwa hivyo kufanya hivyo ni kuyatweza. Kilicho wajibu ni kwamba yakusanywe na yahifadhiwe kwenye makabati, yachomwe moto au yazikwe. Ama kuyatumia kuswalia juu yake, kuyafanya meza ya chakula au kufungia mahitaji, hilo ni jambo lisilojuzu. Kwa sababu mara nyingi hayakosi kuwa na Aayah. Ama likipatikana gazeti ambalo halina kitu, halina utajo wa Allaah, Aayah wala chochote, basi hakuna ubaya. Lakini ni nadra kupatikana gazeti katika nchi hizi lisilo na chochote cha utajo wa Allaah, Aayah au Hadiyth. Hivyo haitakikani wala haijuzu kuyatweza. Bali lazima lichomwe moto kama halina haja yoyote, lizikwe katika ardhi safi au lihifadhiwe kwenye makabati ili lisidhalilishwe.

Ama picha zilizomo, kuna uwezekano wa kufutwa vichwa vyake na likizikwa bila kuonekana chochote. Hiyo haidhuru. Madhara ni kuonekana kwake na kusambaa kwake au kuliweka juu ya milango na sehemu zingine. Ama likizikwa mpaka Allaah atimize atakavyo ndani yake au likachomwa moto au likazikwa ardhini, basi hakuna tatizo.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1351/حكم-الصلاة-على-ورق-الجراىد
  • Imechapishwa: 14/12/2025