Swali: Je, atafanyiwa hesabu kwa matendo yake mtoto ambaye ana ugonjwa wa akili?  Je, inahesabiwa mtoto mwenye ugonjwa wa akili kuwa ni adhabu kwa wazazi wake?

Jibu: Mtoto mwenye ugonjwa wa akili humumu yake ni sawa na mwendawazimu; ´ibaadah si zenye kumuwajibikia na wala hatofanyiwa hesabu siku ya Qiyaamah. Lakini ikiwa wazazi wake wawili ni waislamu au ana mzazi mmoja ambaye ni muislamu, basi ana hukumu moja kama wazazi wake. Kwa msemo mwingine ni kwamba mtoto huyu na yeye anakuwa ni muislamu na hivyo ataingia Peponi. Ama ikiwa mtoto huyu anatokana na wazazi ambao ni makafiri, kwa mujibu wa maoni yenye nguvu,  ni kwamba atapewa mtihani na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa yale anayoyataka. Akiitikia na kutekeleza, ataingia Peponi, na akiasi, ataingia Motoni. Haya ndio maoni yenye nguvu juu ya watu aina hii. Wanayo hukumu hiyohiyo wale watu ambao hawakufikia na ulinganizi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama wale watu wanaoeshi mbali kabisa na miji ya Kiislamu na hawakusikia chochote juu yake; Allaah (Subhaanah) siku ya Qiyaamah atawafanyia mtihani kwa yale anayoyataka; yule mwenye kutii katika wao ataingia Peponi na ambaye ataasi ataingia Motoni.

Pengine mtu akaulizwa ni vipi watapewa mtihani ilihali wako katika ulimwengu wa malipo na hawako katika ulimwengu wa makalifisho. Ndio, mosi ni kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anafanya akitakacho. Anayo haki ya kuwakalifisha waja Wake huko Aakhirah kama ambavo aliwakalifisha ulimwenguni. Pili ni kwamba makalifisho Aakhirah ni jambo limethibiti kwa andiko wazi la Qur-aan:

يَوْمَ يُكْشَفُ عَن سَاقٍ وَيُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ فَلَا يَسْتَطِيعُونَ خَاشِعَةً أَبْصَارُهُمْ تَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ ۖ وَقَدْ كَانُوا يُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ وَهُمْ سَالِمُونَ

”Siku utakapofunuliwa Muundi na wataitwa kusujudu lakini hawatoweza. Macho yao yatainama chini, utwevu utawafunika na hali ya kuwa walikuwa wakiitwa wasujudu walipokuwa wazima wa afya.”[1]

Mfano wa mambo kama haya yanaweza kutokea Aakhirah.

Kwa hivyo mtoto huyu mwenye ugonjwa wa akili hukumu yake ni sawa na wendawazimu na ´ibaadah si yenye kumuwajibikia. Vilevile ana hukumu sawa na wazazi wake.

Kuhusu sehemu ya pili ya swali, hakika wakati fulani mitihani inakuwa ni adhabu na wakati mwingine inakuwa ni majaribio. Mtu anapofanya jambo la haramu au akaacha jambo la wajibu, basi anaweza kuharakishiwa adhabu duniani na akafikwa na janga Alitakalo. Wakati mwingine Allaah anaweza kumsibu mtu na janga, sio kwa sababu ya adhabu ya kuacha jambo la wajibu au kwa sababu ya kufanya jambo la haramu, bali kwa njia ya kumpa majaribio. Allaah wakati mwingine humjaribu mwanadamu ili kuona kuwa atakuwa mwenye subira au hatokuwa mwenye subira. Akisubiri, basi msiba huo inakuwa ni neema, na sio msiba, na unampandisha katika ngazi za juu zaidi.

[1] 68:42-43

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/18-20)
  • Imechapishwa: 24/03/2026