06 – Bakr bin Hamraan amesema:

“Nimemsikia ´Amr bin ´Ubayd akisema: “Mwizi hasamehewi.” Ndipo nikamtajia Hadiyth ya Swafwaan bin Umayyah[1]. Akasema: “Je, unaapa kwa jina la Allaah ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema hivyo? Nikasema: “Je, unaapa kwa jina la Allaah ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hakusema hivyo? Akaapa kwa jina la Allaah. Nikamuhadithia Ibn ´Awn jambo hilo. Wakati umati wa watu ulipokuwa mkubwa katika darsa akasema: “Ee Bakr! Wahadithie watu!”

07 – Nuuh bin Qays amesema:

“Tulikuwa tumeketi kwenye nyumba ya familia ambayo ilikuwa imempoteza jamaa wakati ambapo ‘Amr bin ´Ubayd alipotujilia. Tulikuwa tunazungumzia juu ya Hadiyth ya Bahz bin Hakiym ambapo bwana mmoja aliiamuru familia yake kuuchoma moto mwili wake baada ya kufa na kutupa majivu hewani na kwamba Allaah atamkusanya na kumleta. ‘Amr akasema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kamwe hakusema hivo. Ikiwa amesema hivyo, basi mimi namkadhibisha. Ikiwa ni dhambi kumkadhibisha, basi mimi nitaendelea kumkadhibisha.”

08 – Quraysh bin Anas amesema:

”´Amr bin ´Ubayd ametuhadithia… Nini kitatokea kwa ´Amr bin ´Ubayd? Konzi ya mchanga ni bora kuliko yeye.”

09 – Sa´iyd bin ´Amir amepokea kutoka kwa bwana mmoja aliyemtaja jina ambaye amesema:

“Nilikuwa kwa Yuunus bin ‘Ubayd alipomjilia mtu mmoja na kumwambia: “Unatukataza kuketi na ´Amr bin ‘Ubayd na mimi namuona mwanao akifanya hivyo.” Haukupita muda mrefu mtoto wake akaletwa. Yuunus akasema: “Ee mwanangu mpendwa! Unaona nakataza watu kukaa na Amr bin ´Ubayd wakati wewe mwenyewe unakaa naye?” Akasema: “Ee baba mpendwa! kukaa naye wala sikukusudia kufanya hivo. Alikuwepo kwake bwana mmoja na nilikuwa na haja naye. Ndio maana nikamwendea bwana yule.” Yuunus akasema: “Ee mwanangu mpendwa! Nakukataza zinaa, wizi na unywaji pombe, lakini afadhali tukutane na Allah na madhambi hayo kuliko kukutana na Allaah tukiwa na maoni ya ´Amr bin ´Ubayd na wafuasi wake.” Akayakariri maneno hayo mara kadhaa.”

10 – Yuunus bin ´Ubayd amesema:

“´Amr bin ‘Ubayd alikuwa akisema uwongo wakati anpopokea Hadiyth.”

[1] Sufyaan bin Umayyah amesema:

“Nilikuwa nimelala msikitini ndani ya kanzu yangu ambayo iligarimu sarafu thelathini za fedha. Mtu mmoja akaja na kuniibia. Mtu huyo akakamatwa na kupelekwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ambaye aliamrisha kukatwa mkono wake.” Nikaenda kwake na kusema: “Je, utaukata mkono wa mtu huyo kwa vipande thelathini vya fedha? Sitaki hivo.” Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Endapo ungesema hivyo kabla ya kuja kwangu pamoja naye.” (Abu Daawuud (4/553), an-Nasaa’iy (8/61) Ibn Maajah (2/865))

  • Muhusika: Imaam ´Aliy bin ´Umar ad-Daaraqutwniy (afk. 385)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Akhbaar ´Amr bin ´Ubayd bin Baab al-Mu´taziliy, uk. 91-96
  • Imechapishwa: 22/11/2025