Swali: Kila wakati kunapotokea mizozo kati yetu basi mume wangu ananitisha kwa kunituma kwenda katika nyumba ya familia yangu. Hili hutokea kwa wingi wakati mume na mke wamegombana. Ni zipi nasaha zako, ee Shaykh, kwa wale ambao hii ndio tabia yao khaswa ukizingatia ya kwamba Allaah (Jalla wa ´Alaa) amemkataza mwanamke kutoka nyumbani kwa mume wake hata kama ametalikiwa?

Jibu: Nasaha zangu kwa waume hawa ni kwamba wanatakiwa kuwa wanaume kama ambavyo wako hivo na wawe na usimamizi katika nafsi zao na wasiwe ni wenye kusahau wakati wa hasira. Kuna mwanaume alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amuusie ambapo akamwambia: “Usikasirike.” Akarudi mara kwa mara akamwambia: “Usikasirike.”

Suluhu ya kutatua matatizo kati ya mume na mke sio kwa kumfukuza kutoka nyumbani na kwenda katika familia yake. Hili halizidishi jengine isipokuwa matatizo zaidi. Kinachotakikana ni yeye ampende mke wake na amsamehe makosa yake. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muumini mwanaume asimchukii muumini mwanamke. Kwani akichukia kutoka kwake tabia fulani basi atapendezwa na nyingine.”

Kinachotakikana ni mwanaume awe mwanaume wa kisawasawa. Nikimaanisha hivo kweli. Ni nani ambaye huthubutu kusahau mema wakati kunapotokea kosa moja? Ni mwanamke. Je, hivi kweli unataka kuishusha nafsi yako mpaka uwe katika ngazi ya mwanamke ambaye anapoona kosa moja kutoka kwa mume wake basi humwambia:

“Mimi sijapatapo kuona kheri yoyote kutoka kwako.”

Kwa ajili hiyo ninawanasihi ndugu zangu pindipo kunatokea matatizo au kuelewana makosa kati ya na wake zao, basi mume awe na subira na ustahamilivu. Atangamana na mwanamke vile anavostahiki kwa mujibu wa vile alivyousia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Hakika wao wameumbwa kutokana na ubavu. Kiungo kilichopinda zaidi ni kile cha juu. Ukisema ukinyooshe basi utakivunja. Ukistarehe naye basi utastarehe naye juu ya kupinda kwake.”

Hivi ndivo kasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Mimi naamini kuwa mwanamume akimtii Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kutangamana kwa uzuri na mke wake, basi Allaah atageuza ule uadui na chuki uliyomo moyoni mwake na kwenda katika mapenzi na mahaba. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

لَا تَسْتَوِي الْحَسَنَةُ وَلَا السَّيِّئَةُ ۚ ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيمٌ

”Na wala haulingani sawa wema na uovu; lipiza [uovu] kwa ambalo ni zuri zaidi. Tahamaki yule ambaye kati yako na yeye kuna uadui, atakuwa kama ni rafiki mwandani.”[1]

Nyoyo ziko mikononi mwa Allaah (´Azza wa Jall). Lipiza uovu kwa ambalo ni zuri zaidi na utaona mambo yatavyobadilika.

[1] 41:34

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (38) http://binothaimeen.net/content/870
  • Imechapishwa: 06/07/2018