Swali: Kuwatukana wanachuoni kunamtoa mtu katika Uislamu?

Jibu: Ikiwa anawatukana kwa sababu ya ´Aqiydah yao kunamuharibia mtu ´Aqiydah yake. Ama ikiwa anawatukana kwa chuki binafsi na hasadi ni dhambi kubwa. Hata waislamu wa kawaida ni haramu kuwatukana na kuwatupia tuhuma. Damu, mali na heshima ya muislamu ni haramu. Tusemeje kuhusu wanachuoni? Wanachuoni wana haki kubwa zaidi kuliko watu wa kawaida. Pindi kundi la watu katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliposema, huku wakidai kuwa wanafanya mzaha na wanacheza:

“Hatujaona kama wasomaji wetu hawa! Wana matumbo makubwa, ndimi zao zinasema uongo sana na ni waoga wakati wa kupambana na maadui.”

wakimaanisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake. Allaah akateremsha juu yao:

وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَلَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Ukiwauliza basi watasema: “Hakika tulikuwa tunafanya porojo na tunacheza.” Sema:  “Je, mlikuwa mnamfanyia mzaha Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?” Msitoe udhuru, mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (09:65-66)

Mambo ni khatari sana. Mtu ambaye anawatukana wanachuoni kwa sababu ya ´Aqiydah yao sahihi na kulingania kwao kwa Allaah kuna khatari akawa ni miongoni mwa wanafiki na akaingia kwenye tabaka ya chini kabisa Motoni. Ikiwa anawatukana kwa sababu ya hasadi au chuki binafsi ni dhambi kubwa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Masaa´il-il-Jaahiliyyah (01) http://alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/jahlyh_01.mp3
  • Imechapishwa: 18/11/2017