Swali: Ni upi mtazamo wenu kuhusu baadhi ya vipindi vya runinga vinavyowasilisha maigizo ya kidini, wakiigiza Maswahabah, wanafunzi wa Maswahabah na maimamu?

Jibu: Tayari hili limeshajibiwa mara kadhaa. Tayari limejadiliwa katika baraza la wanazuoni wakuu na baraza la misingi la jumuiya na mengineyo. Wote wamekubaliana kuwa kuwaigiza Maswahabah na Mitume haijuzu kabisa. Hili lina madhara mengi na linaweza kusababisha uwongo juu yao, kuwasilishwa katika sura isiyo nzuri na isiyowastahili, kupelekea dharau na mzaha juu yao. Kwa hivyo haijuzu kabisa kuwaigiza Mitume wala Maswahabah katika sehemu yoyote.

Kuhusu wengine wasiokuwa wao, hilo linahitaji kutizamwa. Huenda likafaa katika baadhi ya mambo endapo lengo ni kheri na manufaa ya ummah wa waislamu, na huenda lisifae kwa sababu ni uwongo na uzushi. Kwa jumla maigizo ni jambo la kutizamwa na kufafanuliwa. Baadhi ya watu huliona kuwa halina kosa ikiwa lina manufaa ya jumla. Kwa mfano mtu anawasilishwa kama mwenye kusimamia matendo mema, anayekataza maovu, akizungumza kwa niaba yake katika maamrisho na makatazo kana kwamba ndiye huyo. Wengine hujengea hoja kwa mfano kuja kwa Jibriyl katika sura mbalimbali, kama alivyoonekana katika umbo la bedui, katika umbo la ´Urwah bin Mas´uud na katika umbo la Dihyah bin Khaliyfah al-Kalbiy na maumbo mengine. Alifanya hivo kutokana na hekima za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hivyo suala la maigizo linahitaji kutazamwa upya na kuchunguzwa kwa kina pande zake zote.

Kuhusu kuchora au kuunda picha kama picha ya mtu fulani, kama picha ya ´Umar au mtu fulani, hilo halijuzu. Picha hazijuzu kamwe. Bali kinachozungumzwa hapa ni maigizo yasiyo na taswira. Mtu kusimama na kujifanya kama yeye ndiye ´Umar, Maalik, ash-Shaafiy´iy, Ahmad, al-Awzaa´iy, Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab au ´Abdul-´Aziyz akizungumza. Kwa maana nyingine anawakilisha bila picha. Hapo ndipo kuna mahala pa kuchunguza kama inafaa au haifai.

Ama kumhusishia hilo Jibriyl ni kutokana na amri ya Allaah. Hakutumiwi kama kipimo. Jibriyl alikuja kwa haki, ni mwenye kuwajibishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) katika sura hizo kwa hekima maalum ili watu wanufaike na waone anayekuja kuuliza na kuzungumza na hivyo faida kuwa kubwa zaidi kwao. Hili ni jambo maalum ambalo nayaona halifai kulinganishwa kwa jambo jingine katika uigizaji wa Jibriyl na kuja kwake kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1020/حكم-وخطر-تمثيل-شخصيات-الانبياء-والصحابة
  • Imechapishwa: 06/01/2026