Yule ambaye anamwamini Allaah na siku ya Mwisho haifai kwake kukomeka kwa mwalimu mmoja peke yake, pasi na kujali ni mzuri, heshima, msomi na mwema kiasi gani. Muislamu anatakiwa kuwa kama nyuki ambaye anaruka kutoka katika mti hadi mwingine, kutoka katika ua hadi jengine, akatoa katika matumbo yake kinywaji na baadaye akazalisha asali ambayo watu wanajitibu kwayo. Namna hii ndivo anavyotakiwa kuwa muislamu. Anatakiwa kuchukua elimu kutoka kwa kila mwanachuoni. Hivo ndivo walivyokuwa wakifanya wanachuoni wa Salaf (Rahimahumu Allaah). Walikuwa wanaweza kuwa na mamia ya waalimu.

Kwa mfano inasemekana kwamba Imaam Abu Haniyfah (Rahimahu Allaah) alikuwa na waalimu 1000. Sio jambo muhimu kama simulizi hii imesihi au haikusihi.

at-Twabaraaniy amepangilia kitabu chake ”al-Mu´jam as-Swaghiyr” kutokana na majina ya waalimu wake. Mpangilio huu ndani yake kuna sanaa. Amewapangilia kutokana na mpangilio wa kiherufi na akasimulia Hadiyth moja kutoka kwa kila mwalimu. Alikuwa na waalimu wangapi? Zaidi ya 1000. Haya yameandikwa katika ”al-Mu´jam as-Swaghiyr” yake. Lengo lake ilikuwa kuhifadhi majina ya waalimu wake. Vinginevyo anavyo vitabu vitatu: ”al-Mu´jam as-Swaghiyr”, ”al-Mu´jam al-Awsatw” na ”al-Mu´jam al-Kabiyr”. Hivyo viwili vya mwanzo usulubu wake ni mmoja, bi maana kwa mpangilio wa waalimu wake. Tofauti pekee ni kwamba katika ”al-Mu´jam al-Awsatw” hutaja zaidi ya Hadiyth moja kutoka kwa waalimu wake. Kwa hivyo alikuwa na zaidi ya waalimu 1000. Namna hii ndivo walivokuwa wanachuoni wa kale. Kwa sababu ukweli wa mambo ni kwamba kila mwanachuoni anayo sifa ya kipekee inayotofautiana na mwenzake inapokuja ima katika elimu, tabia, dini, wema na mfano wa hayo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Raabigh (5)
  • Imechapishwa: 08/11/2020